Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana walitema cheche katika shughuli ya kuaga mwili wa mbunge wa zamani wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo.
Mawaziri hao katika salamu zao za rambirambi walielezea masikitiko yao juu ya chuki kubwa inayopandikizwa nchini na pia jitihada zinazoendelea za kukandamiza demokrasia.
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyehudhuria shughuli hiyo hali ambayo ilionekana kuibua minong’ono kwa baadhi ya waombolezaji.
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia alienda mbali zaidi na kusema hakukuwa na uwakilishi wa CCM unaofanana na sifa ya Ndesamburo aliyependa amani.
Katika hafla hiyo ya kumuaga kitaifa iliyofanyika uwanja wa Majengo, wabunge wa CCM waliwakilishwa na mbunge wa viti maalumu, Ester Mmasi aliyedai kuiwakilisha pia CCM.
Hotuba ya Mbowe
Hotuba ambayo iligusa hisia za waombolezaji wengi ni ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema hatua ya viongozi wa Serikali na CCM kutohudhuria si tukio la bahati mbaya.
“Leo tumejenga Taifa lenye hofu. Watu wamekuwa waoga kwa sababu viongozi wameingiza hofu katika Taifa letu. Watu wenye hatia wana hofu. Kukosekana kwa uwakilishi wa Serikali mahali hapa si ajabu,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Ni hofu ya hatia. Kwa heshima sana dada yangu Mmasi (Ester) pole. Asante sana kwa kufika. Umekuja hapa na kujaribu sana unamwakilisha sijui Serikali, sijui Rais. Hakuna.”
Mbowe alisema ameona vituko vingi katika msiba wa Ndesamburo kiasi kwamba anajiuliza inakuwaje wakati alikuwa mtu mwema na walitamani hata kumsindikiza kwa bendi ya polisi. “Tukaenda Chuo cha Polisi kuomba bendi ambacho mzee (Ndesamburo) anawasaidia mambo mbalimbali. Brass band hii inakodishwa kwa Sh300,000, tulikuwa tayari kulipa gharama hiyo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Mkuu wa chuo anaogopa kutoa Brass band ananiambia mwenyekiti Mbowe ongea na IGP (mkuu wa Jeshi la Polisi). Yaani Mbowe nimpigie IGP simu kumuomba Brass band (bendi ya polisi), mimi?”
“Leo polisi wanaogopa kufanya kazi kwa sababu hawajui bwana mkubwa atafurahi ama atakasirika. Ni mambo ambayo si ya Kitanzania. Tukahitaji kiwanja cha kumuaga baba nacho tukanyimwa.”
“Si kwamba kiwanja hiki cha Majengo hakifai. Ila kwa historia ya Moshi, uwanja wa Mashujaa kama unavyoitwa unastahili kuwa uwanja wa kuagwa mzee wetu Ndesamburo. Polisi wakaweka mizengwe.”
Mbowe alisema alifanya juhudi kubwa ikiwamo kuwasiliana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alimueleza kuwa anashughulikia, lakini hata hivyo ilikuwa ahadi hewa.
“Tulisema baba yetu ni kiongozi wa watu na sio wote wataweza kuja uwanjani. Tukaona ni haki tumpitishe (Ndesamburo) katikati ya mji lakini usiku tukaletewa barua ya zuio la polisi,” alisema.
“Kuna kiburi kinajengwa sana mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Naomba nimpelekee salamu mheshimiwa Rais, Watanzania wote sisi ni ndugu,” alisisitiza Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai.
“Mwalimu (Nyerere) alitujenga tukawa tunapendana, lakini utawala huu wa awamu ya tano unafanya matendo yanayoonyesha ubaguzi na tunaona uonevu usiohimilika kwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha”.
Mbowe alisema ingawa watu wengi wanaogopa kuyasema hayo, yeye atayasema ili Rais, Waziri Mkuu na Serikali nzima ielewe kuwa Kilimanjaro na Arusha ni sehemu ya Tanzania.
“Watu wengi wanaogopa kusema. Siku hizi hata unaogopa kusema wewe ni Mushi. Uongo? Siku hizi watu wanaogopa kujiita Masawe, kujiita Tarimo kwa sababu huna uhakika watawala watafanya nini.”
“Hatuhitaji kujenga Taifa lenye ubaguzi, tunahitaji kumheshimu na kumthamini kila Mtanzania bila kujali dini yake, kabila lake wala jinsia. Tumuenzi Ndesamburo kwa kupendana,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema Ndesamburo katika uhai wake alifanya mambo mengi na alikuwa mfadhili mkubwa si kwa Chadema pekee, bali watu wengi na makundi mbalimbali.
“Wakati polisi wanakuja kutufukuza katika uwanja wa Mashujaa na mabomu. Tukawaambia gari mnaloendesha tairi amenunua Ndesamburo. Na ni ukweli, sio nasema maneno ya uongo.”
“Huyu baba amejenga Mawenzi (hospitali) nani asiyejua. Amesaidia taasisi mbalimbali za dini, Wakristo na Waislamu. Amesaidia mashule sio tu kwa mkoa wa Kilimanjaro hata mikoa mingine.”
Mbowe alisema pamoja na kujitoa kwake huko, wako watu wanashindwa kuona thamani yake kwa sababu ya itikadi za kisiasa na kusisitiza kuwa siasa ni mambo ya mpito, lakini jamii itabaki.
“Leo sisi tunazika huku, bungeni wanamsimamisha Halima Mdee na Ester Bulaya. Hatuwezi kujenga Bunge la vibogoyo. Hatuwezi kujenga Bunge la wabunge waoga,” alisisitiza kiongozi huyo wa upinzani.
“Hii nchi imefika hapa kwa sababu kuna watu waoga na wenye hofu. Ugomvi wa Ester Bulaya na Halima Mdee ulianza wakati wa bajeti ya Nishati na Madini.”
“Katika mjadala ule mheshimiwa Mnyika (John) kaamriwa kutoka nje na spika kwa uonevu ulio dhahiri. Wabunge wale akina mama wakasimama wakasema huyu mtu hatendewi haki. Wabunge msifungwe midomo na mkienda bungeni wabunge wote msimame imara na Watanzania bila kujali vyama vya siasa tuitake nchi hii ijifunze kuhoji viongozi wanapofanya makosa.”
Mbowe alitumia hadhara hiyo kutuma salamu kwa wale aliosema wanafikiri kuondoka kwa Ndesamburo ni kuterereka kwa Chadema akisema haitatokea na wataendelea kuijenga vyema Moshi.
Sumaye, Lowassa na Mbatia
Sumaye ambaye ndiye aliyeongea kwa kirefu alisema Afrika itaendelea kama Serikali zilizo madarakani zitaenzi demokrasia na kuachia madaraka kwa amani badala ya kung’ang’ania.
“Kuna juhudi kubwa sana zinaendelea za watu kujidanganya kuwa wanaweza kukandamiza demokrasia. Hapa demokrasia ilipofikia huwezi tena kuikandamiza,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Mpira una bladder (puto) ndani. Ukiikandamiza sana itapasuka na ikipasuka itakuwa na madhara makubwa. Tuache Watanzania wafurahie demokrasia katika nchi yao. Hili ni muhimu.”
“Tuache kupandikiza chuki. Mikutano ya siasa inazuiwa, njia za kupitisha maiti (ya Ndesamburo) zinazuiwa. Hatuwezi kuwaonea wananchi hawa kwa muda mrefu.”
Lowassa aliunga mkono maneno yaliyosemwa na Sumaye kuhusu jitihada kubwa zinazoendelea za kudidimiza demokrasia na kupandikiza chuki katika jamii.
“Jitihada za kudidimiza demokrasia inaendelea sana. Hawa waliozuia tusiagie Mashujaa tuwasamehe. Hupimi watu kwa uwanja, bali kwa roho zao,” alisema Lowassa aliyegombea urais mwaka 2015 kupitia Ukawa.
Awali, katika hotuba yake Mbatia alilaani tabia iliyoanza kujengeka ya kuwafarakanisha Watanzania na kumtaka Rais Magufuli ajue kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) alitoa mfano wa tukio la Aprili 30, wakati Rais alipofanya ziara mkoani Kilimanjaro ambapo meya na mbunge walitimuliwa Ikulu.
“Mbunge wa Moshi Mjini (Jaffar Michael) na meya wa Moshi (Raymond Mboya) wakaondolewa Ikulu na Rais akakaa kimya tu. Tanzania ni mali ya Watanzania na sio ya John Pombe Magufuli,” alisema.
“Tangu tumeanzisha mageuzi haya labda John Magufuli alikuwa shule, lakini hatuwezi kukubali Taifa letu likasambaratika kwa maslahi ya watu wachache,” aliongeza kusema na kusisitiza:
“Rais akija Moshi, mwenyeji wako ni meya na mbunge, watu wako wa usalama hawawezi kuwaondoa.
“Niwaombe CCM, Tanzania ni mali ya Watanzania wote, nitaongea nao. Kitendo walichofanya leo sio utamaduni wa Watanzania. Sioni uwakilishi wa CCM unaofanana na Ndesamburo.”
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Severina Mwijage alisema wale wote waliozuia Ndesamburo asiagwe katika Uwanja wa Mashujaa Mungu atawalipa kwa kile walichokifanya.
“Huwezi kuwachonganisha wananchi namna hii. Chadema mna salamu inasema peoples power. Tungeamua kutumia nguvu ya umma msingeweza (polisi) kufanya lolote,” alisema.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alipendekeza halmashauri ya manispaa ya Moshi inayoongozwa na Chadema kutafuta mtaa bora ndani ya mji na upewe jina la Ndesamburo.
Zitto alisema hiyo itakuwa ni njia bora ya kuenzi mchango mkubwa wa Ndesamburo katika jimbo hilo ili mtu yeyote akifika Moshi ajue jabali la siasa alikuwa anaishi mjini humo.
Katika shughuli hiyo ya kuaga mwili wa Ndesamburo, waziri wa zamani wa fedha na mbunge wa zamani wa Rombo (CCM), Basil Mramba alikuwa kivutio alipoingia uwanjani hapo.
Gwajima aliamsha ‘dude’
Askofu mkuu wa Kanisa la Ufufuo, Josephat Gwajima alimshukia mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa kile alichodai kuingiza siasa katika misiba.
Askofu Gwajima ambaye alisema anataka kuitibu Moshi na Arusha, alisema amepata tetesi kuwa Gambo ndiye aliyezuia Ndesamburo asiagwe Uwanja wa Mashujaa.
Alienda mbali na kumsihi Rais Magufuli kumwajibisha Gambo kwa kuingiza siasa katika msiba wa Ndesamburo akisema anaamini Rais hakumtuma kufanya hivyo.
“Tetesi ni kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa maelekezo, amekataza kufanyia Uwanja wa Mashujaa kwa sababu ya sauti kubwa sana kwamba kuna mahakama na kuna shule,” alisema.
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei alimuelezea Ndesamburo kama mtu waliyeanzisha naye chama wakati huo kikiwa hakina mwanachama hadi sasa Chadema ni chama kikuu cha upinzani.
“Nilibahatika kuasisi chama hiki cha Chadema wakati huo nilimfahamu ndugu yangu, rafiki yangu Philemon Ndesamburo. Tulikuwa wote pale Oysterbay na tulijenga sehemu inayoambatana,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Chadema, Bulaya alisema Ndesamburo ndiye aliyemshauri aondoke CCM na aungane na vijana wenzake kuleta mageuzi ya kweli. “Yeye ndiye aliyeniomba niungane na vijana wenzangu kuleta mageuzi ya kweli. Aliniambia huko uliko siko. Aliniita na kunitia moyo kuwa nitaweza. Akaniambia ungana na vijana wenzako,” alisema.
“Alinitia moyo akaniambia kama mimi (Ndesamburo) nilishindana na shemeji yake Rais (mstaafu Benjamin Mkapa) na nikashinda, wewe ambaye bado ni kijana na una nguvu huwezi kushindwa.”
No comments:
Post a Comment