Monday, June 12, 2017

HIVI PUINDE: Usipate shida msomaji wangu Nimekusogezea Hotuba ya Msemaji mkuu wa kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Halima Mdee, Mengi yaliyoangaziwa ni pamoja na Hali ya uchumi wa Taifa na Mpango wa maendeleo ya taifa kwa mwaka wa fedha 2017/2018

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI   KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA  MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
Image result for fedha_________________________
UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb), naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni hayo, napenda kutumia  fursa hii, kipekee kutoa pole nyingi kwa CHADEMA FAMILY, kwa kuondokewa na mmoja wa waasisi wa CHADEMA, Mzee Philemo Ndesamburo, aliyefariki dunia tarehe 31 Mei, 2017 huko Moshi, Kilimanjaro na hatimaye kupumzishwa katika nyumba yake ya milele tarehe 6 Juni, 2017. Marehemu Mzee Philemon Ndesamburo licha ya kuwa mwasisi wa CHADEMA, lakini pia alijitoa kwa hali na mali kukifadhili na kukilea Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kukifikisha hapa kilipo leo. Mafanikio tuliyo na yo leo kama chama, na kama wabunge wa CHADEMA na viongozi wa chama kwa ngazi mbali mbali, na mafanikio tuliyo nayo leo, katika siasa za vyama vingi hapa nchini,  kwa sehemu fulani yanatokana na juhudi za Mzee wetu huyu.
Mheshimiwa Spika, Taifa limempoteza mwanamageuzi wa karne, aliyekuwa tayari kupoteza maisha yake, kwa ajili ya mabadiliko ya kweli ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Taifa letu. Kama chama, tutamkubuka kwa kuyaenzi yale yote aliyoyaasisi kwa mustakabali mwema wa chama chetu na Taifa kwa jumla. Hakika ni vigumu kuziba pengo aliloliacha. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, AMINA.
Mheshimiwa Spika, baada ya salama hizo za rambi rambi, naomba nitambue mchango uliotukuka wa Mhe. Halima James Mdee (Mb) ambaye ndiye Waziri Kivuli mwenye dhamana ya kuisimamia Serikali katika masuala ya Fedha na Mipango, kwa kufanya kazi usiku na mchana kufanya tafiti na uchambuzi wa nyaraka mbalimbali na kupata takwimu ambazo zimejenga msingi wa hotuba hii kwa zaidi ya asilimia 90.
Mheshimiwa Spika, tofauti na nchi zilizoendelea ambapo watu wenye upeo na weledi wa kufanya kazi namna hii huenziwa na kujengewa mazingira mazuri ya kuwa bora zaidi, katika nchi zinazoendelea watu wa aina hii hukumbana na madhila mengi ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa sababu tu ya ujasiri wao wa kuisimamia na kuikosoa Serikali tena katika misingi ya kikatiba na kisheria.
Mheshimiwa Spika, wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb) anahitimisha hotuba yake kuhusu Bajeti ya Serikali hapa Bungeni tarehe 6 Aprili, 2017 alisema kwamba:  ili maendeleo ya kiuchumi yaweze kumfikia kila mwananchi ni lazima uchumi huo uwe shirikishi. Uchumi huo hauwezi kuwa shirikishi ikiwa tunabaguana kwa misingi ya tofauti za kisiasa au tofauti nyinginezo. Uchumi wa nchi yetu hauwezi kujengwa na kundi moja la jamii na kulibagua linguine. Hali kadhalika uchumi wa nchi yetu hautajengwa na chama kimoja cha siasa kwa kukibagua kingine au kuchochea migogoro ndani ya vyama vingine. Mshikamano wa kitaifa ni muhimu sana katika kujenga uchumi ulio imara. Ndoto ya kufikia uchumi wa viwanda haiwezi kufikiwa tukiwa na msigano wa namna hii.  Aidha, aliongeza pia kwamba: kutofautiana kifikra ni afya ya akili, na ili uvumbuzi utokee lazima kuwe na fikra mbadala  alternative thinking Nilidhani kuwa Serikali na Chama cha Mapinduzi wangetambua kuwa uwepo wa watu wenye fikra mbadala katika taifa hili ni tuna na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; lakini badala yake Serikali wameona kuwa uwepo wa watu hao ni kama mwiba na kikwazo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kunukuu maneno ya Kitabu cha mwasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini Hayati Nelson Mandela No Easy Walk To Freedom kama maneno ya faraja kwa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni waliopatwa na madhila mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na kufungiwa kuhudhuria vikao vya bunge au kuadhibiwa kwa namna nyingine yoyote ile, wakati wakitekeleza majukumu yao ya kibunge,  kwamba wasifadhaike; kwa kuwa imewapasa kupitia njia hiyo, ili kufikia lengo lililo kubwa zaidi la kutwaa madaraka ya dola kwa njia ya kidemokrasia.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba nitoe Bashraff ya Bajeti ya Serikali iliyowasilisha mbele ya Bunge lako kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuungana na waheshimiwa Wabunge ambao kwa umoja wao walisema kuwa bajeti hii haijawahi kutokea katika historia ya hivi karibuni ya bajeti za Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kwamba ni kweli haijawaji kutokea bajeti ya namna hii na kwamba bajeti hii imevunja rekodi kwa sababu zifuatazo:-
Bajeti hii ni bajeti ambayo takwimu za  vitabu vyake vya mapato na matumizi (Volume I, II, III &IV) zinatofautiana sana,  na pia sura ya bajeti iliyosomwa na Mheshimiwa  Waziri wa Fedha na Mipango inatofautiana pia na vitabu hivyo.  Wakati kitabu cha Mapato ya Serikali kinaonyesha kuwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 itakusanya jumla ya shilingi trilioni 23.9; kitabu cha Matumizi ya Serikali kinaonyesha kuwa Serikali inakusudia kutumia jumla ya shilingi trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya shilingi trilioni 3 ambayo vyanzo vyake havijaonyeshwa kwenye kitabu cha mapato. Wakati huo huo, sura ya bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango inaonyesha kuwa bajeti ya Serikali kwa maana ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni kiasi cha shilingi trilioni 31.7  kiasi ambacho hakionekani popote katika vitabu vya mapato na matumizi ya Serikali. Hali kadhalika kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mikaka Mitano  tarakimu hii ya shilingi trilioni 31.7 inaonekana kwamba ni makisio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19. Hivyo, sasa hivi tunatekeleza mapendekezo ya Mpango kwa mwaka wa fedha 2018/19 na sio 2017/18. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakiri kabisa kwamba haijawahi kutokea!!!


Hii ni bajeti ambayo imedhamiria kuuwa kabisa dhana ya ugatuaji madaraka kwa Serikali za Mitaa (D by D) kwa kuziondolea Serikali za Mitaa madaraka yake ya kisheria ya kukusanya kodi ya Majengo, Kodi ya Mabango na Ushuru wa huduma mijini (City Service Levy) kwa malengo ya kujiendesha, na kurudisha madaraka hayo ya ukusanyaji kodi hizo Serikali Kuu kupitia TRA. Hii inadhihirisha kwamba yote yaliyofanywa  na Serikali za CCM zilizopita na gharama zote zilizotumika kuimarisha madaraka kwenye Serikali za mitaa yailikuwa hayana maana yoyote. Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kwamba haijapata kutokea bajeti ya Serikali yenye lengo la kuuwa Serikali za Mitaa kwa kuzipunguzia madaraka na kuziondolea vyanzo vyake vya mapato.

Hii ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania inawalipisha watanzania maskini wasio na uwezo wa kumiliki magari kodi ya ada ya mwaka ya leseni za magari (Annual Motor Vehicle Licence Fee) kwa kuihamishia kodi hiyo kwenye ushuru wa bidhaa za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa ambapo athari zake ni kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi masikini. Ieleweke kupanda kwa bei ya mafuta kutasababisha kupanda kwa nauli katika sekta ya usafirishaji jambo litakalosababisha kupanda kwa bei za vyakula, kupanda kwa bei za kusaga na kukoboa nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia petrol au dizeli kwa wananchi waishio vijijini, kupanda bei kwa pembe jeo za kilimo, kushindwa kupata nishaati ya mwanga kwa wananchi waishi vijijini kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya taa nk. Kwa maneno mengine bajeti hii imelenga kuwabebesha wananchi masikini mzigo wa kodi kwa matumizi ya anasa ya watu wa tabaka la kati na juu wenye uwezo mkubwa kifedha wa kuweza kumiliki magari na vitu vingine vya thamani kubwa. Katika hili, Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kabisa kwamba haijawahi kutokea bajeti ya namna hiyo ya kuwanyonya masikini na kuwaneemesha matajiri. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani haijawahi kuona chombo chochote cha moto cha usafiri wa barabarani kinachotumia mafuta ya taa.

Hii ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania Serikali itatoza kodi ya shilingi elfu kumi (10,000/=) kwa nyumba zote katika halmashauri zote nchini  ambazo hazijafanyiwa uthamini zikiwemo nyumba za tembe na tope kwa wananchi masikini waishio vijijini. (Hii iko katika ukurasa wa 48 kipengele cha iii cha hotuba ya Bajeti 2017/18) Badala ya Serikali kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili wananchi wa vijijini waweza kuwa na nyumba bora zenye staha, na badala ya Serikali kufanya uthamini wa ardhi na nyumba za wananchi masikini waishio vijijini ili waweze kupata hati miliki itakayoongeza thamani ya ardhi na nyumba zao ili waweze kutumia hati hizo kupata mikopo itakayoboresha maisha yao; bado Serikali imeendelea kuwabamiza kodi katika ufukara na uduni wao. Haya ni mastaajabu!!!, na hakika Kambi Rasmi ya Upinzani haijawahi kuona bajeti ya namna hii.

 Hii ni bajeti ambayo imeendelea kupandisha kodi kwenye bidhaa ambazo uzalishaji wake hutumia malighafi inayozalishwa ndani ya nchi kama vile shayiri, zabibu, tumbaku n.k, jambo ambalo ni dhahiri litapunguza bei za mazao hayo, na hivyo kupunguza kipato cha wakulima wa mazao hayo. Kwa maneno mengine, bajeti hii haimjali mwananchi masikini ambaye ndiye mzalishaji wa malighafi hizo.

 Hii ni bajeti ambayo imejinasibu kama bajeti ya uchumi wa viwanda wakati haijaonyesha popote mkakati wa kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo ndiyo msingi wa uzalishaji  viwandani.

Hii ni bajeti ambayo haijataja popote itaongeza ajira kiasi gani kwa watanzania na wala haijasema itapunguza umasikni wa watanzania wa kiwango gani kwa mwaka wa fedha 2017/18. Aidha, ni bajeti ambayo haikuzungumzia popote utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Spika, wahenga walisema,ukistaajabu ya Musa, utaona ya Firauni. Maajabu ya bajeti hii ni mengi lakini itoshe kusema tu kwamba ukiwa mwongo, basi uwe pia na kumbukumbu nzuri Waheshimiwa wabunge na hata wananchi wanaweza kusahau mengine, lakini hili la ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ni mapema mno kuweza kulisahau. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutolea maelezo ahadi hii ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ili wananchi wajue kama wamekopwa fedha hii au wamedhulumiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, waliosema kwamba bajeti hii haijawahi kutokea walikuwa sahihi, na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaunga mkono.

Mheshimiwa Spika, tofauti na bajeti mbadala za Kambi Rasmi ya Upinzani zilizopita ambazo ziliweka msisitizo katika Ukuaji wa Uchumi Vijijini (Rural Growth) safari hii bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebeba kauli mbiu ya Ukuaji Shirikishi wa Uchumi (Inclusive Economic Growth) ambapo watu wote wanatakiwa kushiriki katika kujenga uchumi katika mazingira yao na pia ukuaji wa uchumi unatakiwa uwaguse watu wote katika tabaka zote.

Mheshimiwa Spika, wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni akiwasilisha hotuba yake kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu hapa Bungeni tarehe 6 Aprili, 2017, alisema kwamba:  “tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikijigamba kuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi ikilinganishwa na serikali za awamu zilizotangulia, lakini kumekuwa na kilio kikuu kwa upande wa wananchi kuhusu hali ya maisha kuendelea kuwa ngumu kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu”. Aidha, alisema kwamba: kilio hiki cha wananchi kinamaanisha kwamba ukuaji wa uchumi unaohubiriwa na Serikali haujawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa nchi hii”.

Mheshimiwa Spika, Kiongozi wa Upinzani alinukuu maneno ya Wanazuoni wa uchumi wanaosema kwamba Growth is inclusive when it takes place in the sectors in which the poor work (e.g. agriculture); occurs in places where the poor live (e.g. undeveloped areas with few resources); uses the factors of production that the poor possess (e.g. unskilled labour); and reduces the prices of consumption items that the poor consume (e.g. food, fuel and clothing).

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo; unatokea katika maeneo ambayo watu masikini wanaishi kwa mfano maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali; unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo kwa mfano nguvukazi isiyo ya kitaalamu; na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ukipima hali ya Tanzania utaona kwamba uchumi wetu sio shirikishi kwa kuwa ukuaji wake hautokei katika sekta ambazo watu masikini wanafanya kazi au maeneo ambayo watu masikini wanaishi. Aidha, ukuaji wa uchumi wetu hautumii nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo na pia ukuaji huo haujapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia. Kimsingi bajeti hii ambayo imeshabikiwa kwamba haijawahi kutokea, iko kinyume kabisa na mahitaji hayo ya ukuaji shirikishi wa uchumi.


MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MIAKA MTATU ILIYOPITA 2014/15  2016/17
Mheshimiwa Spika, wahenga wetu walishasema kwamba Sikio la kufa halisikii dawa Nimeanza na methali hiyo, kwa kuwa, kwa miaka yote ya uhai wa Bunge la Kumi na mpaka bunge hili la kumi na moja, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kubana matumizi kwa kupunguza bajeti ya matumizi  kawaida yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo, lakini kinyume chake Serikali hii ya CCM imeendelea kuongeza bajeti matumizi ya kawaida hata kwa matumizi yasiyo ya lazima  na kupunguza bajeti  ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefanya tathmini ndogo ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa maana ya matumizi ya kawadia na matumizi ya maendeleo kwa miaka mitatu mfululizo iliyopita na kubaini kwamba utekelezaji wa bajeti ya Serikali umeweka matumizi ya kawaida kama kipaumbele kuliko bajeti ya maendeleo ambayo ndiyo dira ya ujenzi wa uchumi katika nchi yetu.  Kwa mfano mwaka 2014/15 utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ulikuwa ni asilimia 40, mwaka 2015/16 asilimia 31.24 na mwaka 2016/17 asilimia 35.26. Ukitafuta wastani wa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa kutumia takwimu hizi kwa miaka tajwa utakuta kwamba utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa miaka hiyo haujawahi kuzidi asilimia 40.
Mheshimiwa Spika, wakati utekelezaji wa bajeti ya maendeleo uko chini ya wastani, utekelezaji wa bajeti ya matumizi ya kawaida yakiwemo matumizi yasiyo ya lazima umebaki kuwa juu. Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2014/15 matumizi ya kawaida yaikuwa ni asilimia 91, mwaka 2015/16 asilimia 81 na mwaka 2016/17 asilimia 68.7. Ukitafuta wastani kwa kutumia takwimu hizi kwa miaka tajwa utakuta bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikitekelezwa kwa kwa takriban asilimia 80.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuweka rekodi sawa kwamba; utekelezaji wa asilimia 68.7 wa  bajeti ya matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2016/17, haumaanishi kwamba Serikali imebana matumizi bali imegoma kutoa fedha ambazo zilikuwa zimepangwa kutumiwa na kwa maana hiyo, fedha hizo zinabaki kuwa ni deni la Serikali. Kwa maneno mengine matumizi ya kawaida bado yako juu ukilinganisha na matumizi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, mwenendo huu wa kutumia mapato yetu kwa matumizi ya kawaida kwa takriban asilimia 80 na kutoa fedha kiduchu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambazo nazo hazitolewi kwa wakati, kunaifanya nchi yetu kuwa na uchumi wa mchumia tumbo  yaani hand to mouth economy.

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Mei, 2017 wakati nawasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha, nilieleza kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa ikipuuza utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo ndiyo msingi wa uchumi wa wananchi kwa kutotoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo. Katika maelezo yangu nilitaja Wizara 10 za mfano kuonyesha tofauti ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge na fedha halisi zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bado Serikali haijatoa sababu za msingi za utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo, nitarudia sehemu hiyo, ili kwa mara nyingine kuipa Serikali nafasi ya kuwaeleza wananchi ina lengo gani hasa kwa kutotekeleza bajeti ya maendeleo kwa takriba asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, Wizara nilizozitolea mfano kwa kutopatiwa fedha za maendeleo kwa ukamilifu wake katika mwaka wa fedha 2016/17 ilikuwa ni kama ifuatavyo:
Ofisi ya Makamu wa Rais  ( Mazingira)
Mheshimiwa Spika, nilieleza kuwa, kati ya  shilingi bilioni   10.9  za miradi ya Maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge katika ofisi hii,  ni shilingi  bilioni 1.2 tu  sawa na asilimia  11.3 ya fedha ya fedha hizo zilizotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa maneno mengine bajeti ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Rais  Mazingira haikutekelezwa kwa asilimia 88.7.
Mheshimiwa Spika, nilitoa angalizo kwamba, fedha hizi ndizo hutumika kupambana na uharibifu wa mazingira yetu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi kama vile ukame, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, njaa nk na kwamba kitendo cha Serikali kutotoa fedha hizo maana yake ni kubariki athari mbaya zinazotokana na uharibifu wa mazingira ziendelee kuwaangamiza wananchi.

Tume ya Kudhibiti Ukimwi :
Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni  10.1 za miradi ya maendeleo  zilizoidhinishwa na Bunge, ni shilingi  bilioni  2.7 tu sawa na asilimia 27  ya bajeti  ndio zimetolewa. Nilieleza kwamba tafsiri ya kutotekeleza bajeti hiyo kwa asilimaia 73, maana yake ni kwamba; vita dhidi ya maambukizi ya UKIMWI hapa nchini si kipaumbele tena cha Serikali hii ya awamu ya tano.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi:
Mheshimiwa Spika, nilieleza pia kwamba, kati ya shilingi bilioni 897.6 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ni shilingi bilioni 500.4 sawa na asilimia 55 ndizo ambazo zilikuwa zimetolewa hadi kufikia Machi, 2017. Hata hivyo, mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba, shilingi bilioni 427 (asilimia 48) zilikuwa ni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na shilingi bilioni 470 (asilimia52) zilikuwa ni kwa ajili ya kugharamia miradi halisi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo katika sekta ya elimu zinaonekana kuwa nyingi kwa kuwa zimechanganywa pamoja na fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwmba; ni muhimu tukatenganisha  kati ya miradi halisi ya maendeleo na  Mikopo ya wanafunzi ili kuweza  kupata picha halisi  ya nini hasa kinakwenda kutumika kutatua changamoto za uboreshaji/ upanuzi/ujenzi  wa miundombinu na shughuliza utafiti  katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, tukija kwenye miradi halisi ya maendeleo, kati ya miradi 16 ambayo ilitengewa fedha  katika mwaka wa fedha  2016/17 Kamati ya Bunge ya Maendelelo na Huduma za Jamii  ilifanya  ukaguzi wa miradi 5 tu sawa na  na 12% ya miradi yote. Kati ya miradi hiyo  mitano , ni miwili tu iliyopatiwa fedha! Tena kwa kiwango kidogo sana. Ifuatayo ni Hali halisi ya miradi mitano iliyokaguliwa  :
Mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)  Mradi namba 6361. Bunge liliidhinisha  shilingi bilioni 4, hakuna fedha yoyote iliyopelekwa
Mradi wa ukarabati wa Chuo Kikuu  cha Dar es salaam  (Mradi namba 6350). Bunge iliidhinisha shilingi  bilioni 9.4, hakuna fedha yoote iliyopelekwa
Mradi wa Hospitali ya Mloganzila (Namba ya Mradi 6364).Chuo kiliomba shilingi 14,549,727,933 (BN. 14.5) hakuna fedha iliyopelekwa mpaka 13/Mei /2017 wakati wa hotuba ya bajeti ya wizara ya elimu inasomwa.
Mradi wa Mfuko wa Utafiti na Maendeleo wa COSTECH (Namba ya Mradi 6345. Katika Malengo ambayo nchi  nchi imejiwekea , ni kutenga 1% ya Pato la Taifa. Hata hivyo, mfuko huu ulitengewa  kiasi cha shilingi  bilioni 12.8 tu  sawa na 0.012% ya pato la Taifa . Pamoja  na udogo huo , kiasi kilichotolewa ni shilingi  bilioni 4.07 tu (sawa na 31.7%). Kati ya hizo fedha Mfuko mkuu wa hazina uliotakiwa kutoa  bilioni 8 ilitoa  shilingi bilioni 1.5 tu na TCRA iliyotakiwa kutoa   shilingi  bilioni 4.8 ilitoa shilingi bilioni 2.57 tu.
Mradi wa ujenzi wa DIT teaching Tower (Namba ya Mradi 4384). Mradi huu una umri wa miaka 11 (2006- 2017)bado unasuasua, hakuna pesa na Matokeo  yake gharama za mradi zimeongezeka  toka bilioni 5 mpaka bilioni 9.

Wizara ya Maji
Tume ya Taifa ya umwagiliaji- Fungu 05:
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Maji, kati ya shilingi bilioni 35.3 za miradi ya maendeleo zilizodhinishwa na Bunge, ni shilingi bilioni 2.9 tu sawa na asilimia 8.4 zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji  wa miradi hiyo. Kwa upande wa usambazaji wa maji ,mijini na vijijini kati ya shilingi bilioni 915.1  zilizotengwa,  zilizotolewa ni shilingi bilioni 181.2 sawa na 19.8% ya fedha  zote za miradi ya Maendeleo ndizo zilizotolewa.
Mheshimiwa Spika, nilisema na narudia tena kusema kwamba; utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo katika sekta ya maji ni matusi kwa watanzania ambao uhaba wa maji umewafanya waishi kama wanyama; na kwamba;  ule usemi wa Serikali wa kumtua mama ndoo ya maji, kwa mazingira haya  ni dhihaka na ni ulaghai   kwa akina mama wote wa nchi hii ambao wanaendelea kusota  na kukumbana na kila aina ya kadhia katika kutafuta maji. Aidha, niliitahadharisha Serikali  Ikumbuke kwamba, hawa kina mama inaowafanyia mzaha kaatika suala la maji  ndio mtaji mkubwa wa kura waliyoipa ushindi, na sasa imeshindwa kutumiza ahadi yake ya kuwatuma ndoo za maji kichwani, kwa kushindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo iliyodhinishwa na Bunge.
Wizara ya Viwanda na Biashara:
Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 42.1 zilizotengwa, wizara ilipokea shilingi bilioni 7.6 tu sawa na 18.6%.  Nileeleza wazi na ninarudia tena kwamba; kwa utekelezaji huo wa bajeti, ni aibu kwa Serikali kutumia Kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda kama kampeni ya kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa:
Mheshimiwa Spika, nilieleza pia kwamba, pamoja na unyeti wa  Wizara hii, bado ilikumbwa na janga hili la kutopewa fedha za maendeleo. Moja ya mradi muhimu sana katika wizara hii  ni mradi wa  Defence Scheme ( mradi namba  6103)  ambao unatekelezwa chini ya  Kifungu namba  2002- Military Research  and Development Fungu 57. Mradi huu, ulitengewa jumla ya shilingi  bilioni 151.1. lakini Mpaka mwezi Machi,2017 wizara ilikuwa imepokea shilingi  bilioni 30 tu sawa na 20%  tu! Mbali na mradi tajwa hapo juu  kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje  Ulinzi na Usalama  fedha za miradi ya maendeleo ziliwasilishwa ni 14.5% tu, yaani Bunge liliidhinisha shilingi   bilioni 230, pesa zilizotolewa  hadi  Machi 2017 ni shilingi bilioni 33.9. Halafu tunaitangazia dunia kwamba tuna lengo la kuwa na jeshi dogo la kisasa lenye weledi, wakati Serikali haitoi fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kupitia miradi hiyo ndiyo tunaweza kuwekeza katika teknolojia ya kisasa na hivyo kuwa na jeshi la kikisasa.
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi:
Mheshimiwa Spika,  Kilimo kiliidhinishiwa shilingi 101,527,497,000 (bilioni 101). Kiasi kilichotolewa ni  shilingi 3,369,416,66 (bilioni. 3.369) sawa na  3.31%. Kwa upande wa mifugo na uvuvi, kiasi cha shilingi 15,873,215,000 (bilioni 15.8) kiasi kilichotolewa  ni bilioni 1.2. Sawa na 8% . Kwa maneno mengine, Kilimo ambacho tunasema kwamba ndio uti wa mngongo wa uchumi wa Tanzania, bajeti yake ya maendeleo haikutekelezwa kwa takriban asilimia 97. Serikali inahubiri Uchumi wa Viwanda ikijua fika kwamba viwanda hivyo haviwezi kuendelea bila ukuaji katika sekta ya kilimo, lakini haitoi fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya Kilimo.  Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba;   ama Serikali imefilisika ila haitaka kukiri hivyo, au kuna tatizo kubwa la afya ya akili (mental health) miongoni mwa watendaji wa Serikali. Tulisema hivyo kwa kuwa  haingii akilini kwamba ile sekta ambayo inategemewa kuleta hayo mapinduzi ya viwanda haipewi fedha za kutosha, halafu Serikali inaendelea kuhubiri viwanda  vitatoka wapi mwenendo huo?
Wizara ya Maliasili na Utalii , fedha za  ndani za miradi ya maendeleo  zilizotengwa ni shilingi  bilioni 2. Fedha zilizotolewa ni shilingi milioni 156,688,000 sawa na 8%
Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa ni shilingi bilioni 25.30 . Fedha zilizotolewa mpaka sasa ni shilingi  bilioni 7.63 tu.
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano:
Mheshimiwa Spika, wizara hii ilitengewa fedha za Maendeleo kwa mchanganuo ufuatao:

Ujenzi iliidhinishiwa shilingi trilioni 2.17 zilizotolewa ni shilingi trilioni 1.07 sawa na asiliia 58.7
Uchukuzi iliidhinishiwa shilingi trilioni 2.49 zilizotolewa ni shilingi bilioni 761.5 sawa na asilimia 30.5
Mheshimiwa Spika, Uchambuzi uliofanywa hapo juu unaonyesha wazi kwamba, ufanisi wa Serikali ya awamu ya tano katika utekelezaji bajeti ya Miradi ya maendeleo na mpango wa kuwaondolea umasikini watanzania  ni  kwa wastani wa  0%- 20%. Wizara pekee iliyoweza kuvuka 50% ni Wizara ya Ujenzi na inafahamika kwamba yapo maslahi mapana yanayohitaji kulindwa katika wizara hiyo.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali hii ya awamu ya tano inashindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo kwa takriban asilimia 70, ni Serikali hii hii ambayo kwa nyakati tofauti imekuwa ikijigamba kwamba imefanikiwa kukusanya mapato kwa kiwango cha hali ya juu kuzidi makisio iliyoyaweka kila mwezi.
 Mheshimiwa Spika, Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba; hizo fedha amabazo Serikali inajisifu kukusanya kwa wingi zinakwenda wapi??  Au zinatumika vibaya  kwa maana ya matumizi ambayo hayajaidhinishwa na bunge? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, ni kwa nini haikutoa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa takriban wizara zote, kwa kisingizio kwamba kulikuwa na upungufu wa fedha lakini wakati huo huo inautangazia umma kwamba imekusanya mapato mengi kuzidi lengo la makusanyo.
Mheshimiwa Spika, Ni Serikali hii hii ambayo kupitia Ilani ya chama chake, na kupitia dira ya taifa ya maendeleo ya 2025 na 2020 kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  imekuwa ikituambia  kwamba suluhisho la kuondokana na hali duni ya uchumi na utegemezi ni kuendesha modernization ya uchumi. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali iliahidi kufanya mambo yafuatayo:
Kutilia Mkazo katika matumizi ya maarifa ya kisasa (Sayansi na Teknolojia)
Kuandaa rasilimali watu katika maarifa na mwelekeo
Kufanya mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi
Kufanya mapinduzi ya viwanda ambavyo ndivyo kiongozi wa uchumi wa kisasa
Mapinduzi  katika nishati na miundombinu ya kisasa
Mheshimiwa Spika, Suala la Msingi ambalo wabunge wa pande zote mbili tunapaswa kutafakari na kujiuliza, kutokana na uchambuzi uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hapo juu, hivi kweli itakapofika 2020 na 2025 malengo (i-v) yatatimia? Na kama nafsi zetu zinatuambia kwamba hayatatimia, tunajipanga vipi kutumia kipindi hiki cha bajeti KUJISAHIHISHA ili mwaka ujao wa fedha TUSIJIULIZE maswali hayahaya?!

HOJA ZA NYUMA ZA KAMBI YA  UPINZANI KUHUSU BAJETI YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti Mbadala za mwaka 2011/12 na 2012/13 Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza masuala kadhaa ili kusaidia kuongeza mapato ya Serikali kwa upande mmoja na kwa upande wa pili kusaidia kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi wa kawaida na hivyo kuboresha maisha yao. Masuala tuliyoyapendekeza ni pamoja na:
Kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia  asilimia moja (1%) ya pato la Taifa kama wenzetu wa Uganda na Kenya.
 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitakiwa kufanya ukaguzi maalum (special audit) katika kitengo cha Deni la Taifa (fungu 22) ili kujua mikopo inayochukuliwa kila wakati inatumika kufanyia nini, na miradi iliyotekelezwa kama ni miradi ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Bado ukaguzi maalum haujafanyika hadi sasa.
Kuongeza Kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma hadi Tsh 315,000 kwa Mwezi. Inashangaza kuwa katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali imeshindwa hata kutangaza nyongeza ya Mishahara licha ya ukweli kwamba hali ya maisha imezidi kuwa ngumu.
Kuifanyia marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwa kufuta sehemu ya Kodi ya Mapato inayotoa fursa kwa kampuni za madini kutumia sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 iliyofutwa (grandfathering). Pendekezo letu lilikuwa na lengo la kutaka kuweka mfumo wa straightline method of depreciation ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya 100 percent depreciation kwenye mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa Corporate Tax. Pendekezo hili ambalo lingeipatia Serikali mapato mengi na kwa sasa bado halijatekelezwa kwa Kampuni za madini zenye mikataba.
Kuanzisha Real Estate Regulatory Authority kama tulivyofanya kwa mwaka uliopita na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili kutokana na biashara ya kupangisha nyumba/vyumba. Serikali bado haijatekeleza pendekezo hili, hakuna sera ya nyumba na hivyo Serikali hupoteza mapato mengi sana kwenye sekta ya nyumba, kodi za nyumba kuwa juu sana na kuumiza vijana wanaoanza maisha na kutozwa kwa mwaka mzima.
Kushushwa kwa tozo ya kuendeleza stadi (Skills Development Levy  SDL) kutoka asilimia sita (6) ya sasa mpaka asilimia nne (4). Katika pendekezo hilo tulishauri kuwa waajiri wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali imechukua pendekezo hili kwenye mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2013/14 lakini bila kuhusisha mwajiri Mkuu, Serikali. Ni vema kodi hii ilipwe na waajiri wote nchini na ishuke kuwa asilimia 4.
Kuwepo na utaratibu wa kuweka stiker maalumu kwa kazi za sanaa zinazotolewa na mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi hizo ili wasanii wanaozitengeneza wanufaike na kazi zao. Pendekezo hili lilikubaliwa na Serikali na hivi sasa TRA na COSOTA wameanza kufanya kazi hii ili kuhakikisha wasanii wetu wanafaidi jasho lao.(ufanisi wake ukoje?)
Kuzuia kabisa kusafirisha ngozi ghafi kwenda nje ya nchi na badala yake kuwe na mpango wa kuziongezea thamani na kuzitumia ngozi ghafi hapa nchini ili kuleta tija katika uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje. Serikali iliamua kupandisha ushuru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Bungeni inaamini kuwa kuna haja kubwa ya kuzuia kuuza mazao ghafi nje ili kukuza ajira za ndani na kuongeza thamani ya mauzo yetu nje.
Kujenga Mazingira ya ukuaji wa uchumi vijijini (Rural Growth) kwa kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, maji na Umwagiliaji. Sambamba na kuundwa  kwa  Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural Development Authority) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.Lengo likiwa kuwe na fedha mahsusi, kutoka chanzo mahsusi zinazotengwa na kuwekewa uwigo (ringfenced ) wa kutotumika kwa shughuli nyingine yoyote zaidi ya kufanya maendeleo vijijini. Pendekezo hili Serikali imelidharau na madhara yake ni kuwa maendeleo ya vijijini hayana uratibu mzuri na hivyo kusahaulika kabisa.
Kukarabati Reli ya Kati na matawi yake.
Kujenga uwezo wa viwanda vya ndani ili kuviwezesha kuzalisha na kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo zilizoongezewa thamani. Tuliitaka serikali kupiga marufuku uuzaji nje wa korosho ghafi kama ilivyovyo kwa ngozi ghafi kwa kuanzia. Serikali haijaweka mkakati wowote wa kuhakikisha korosho yote nchini inabanguliwa kabla ya kuuzwa nje.
Kuboresha elimu na afya hasa kwa shule na zahanati/Vituo vya Afya vilivyo katika maeneo ya vijijini kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wa sekta hizi walio kwenye Halmashauri za Wilaya. Tulipendekeza pia kuanzishwa kwa posho za mazingira magumu. Serikali haijatekeleza pendekezo hili.
Kuanzisha pensheni ya uzeeni kwa wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60. Serikali  ipo kimya kuhusu suala hili muhimu sana kwa wazee nchini.
Tulipendekeza kwamba utaratibu wa vitambulisho vya Taifa uoanishwe na mfumo wa kutoa namba ya utambulisho kwa mlipa kodi (TIN Number) ili kila mwananchi awajibike kujaza fomu za taarifa za kodi  tax returns bila kujali kipato chake. Suala hili lingewezesha kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi nchini na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi. Pendekezo hili bado halijatekelezwa na serikali.
Ilipendekezwa kwamba misamaha yote ya kodi iwekwe wazi na ikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Bajeti ya mwaka 2014/2015 imeridhia pendekezo hili na kuahidi kuwa misamaha ya kodi itawekwa wazi. Utekelezaji wake bado unasuasua!
Kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili kufundisha wataalamu wa kutosha wa sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa Taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo na hivyo kufaidika na utajiri wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu. Serikali ipo kimya kuhusu pendekezo hili kama ambavyo imekuwa kimya KABISA kwenye suala la Mafuta na Gesi katika hotuba   za wizara ya Nishati na Madini na Hotuba ya Bajeti. Wakati miaka michache iliyopita ilikuwa inalipigia upatu kwa mbwembwe  nyingi sana.

HALI YA UCHUMI WA TAIFA -   TAARIFA YA BENKI KUU YA TANZANIA YA  MWEZI  - APRIL 2017  
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwezi Aprili, 2017, hali ya uchumi wa Taifa ilikuwa kama ifuatavyo:
Mfumuko wa Bei: katika Mwezi Machi,  2017 mfumuko wa bei ulikuwa kwa wastan wa 6.4%  ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo  mfumuko ulikuwa kwa 5.4%. Ongezeko husika limesababishwa  na ongezeko la bei ya chakula   kama vile unga, mahindi, mihogo, ndizi, mbogamboga, sukari n.k
Akiba ya chakula:  kwenye ghala la Taifa (National Food reserve Agency  NFRA) kulikuwa na akiba ya chakula ya  tani 86,444. Hii haijumuishi maghala ya watu binafsi.
Mzunguko wa fedha:  Mzunguko wa fedha na upatikanaji wa fedha (Money Supply and Credit ), ulikuwa kwa 4.1% (22,539) mwaka 2017 ikilinganisha na  15.5% mwaka 2016 ( 21,648.5)
Upatikanaji wa  fedha  katika sekta binafsi: Nyongeza ya upatikanaji wa fedha wa sekta binafsi  kutoka kwenye taasisi za fedha ilikuwa  kwa kiwango cha 3.7% kwa mwaka 2017 . Ukuaji ulikuwa wa kiwango cha chini ikilinganishwa  na ongezeko la 23.6% mwezi Machi 2016. Hali hii ni kiashiria cha kusua sua kwa sekta ya fedha nchini na mzunguko /upatikanaji wa fedha kwa wafanyabishara.
Mwenendo wa kibajeti:  Makusanyo ya mwezi Machi, 2017 yalifikia shilingi trilioni 1.45 ikilinganishwa  na shilingi Trillion 1.325 mwaka 2016. Mapato yaliyotokana na kodi  ni shilingi trilioni 1.3  ikiwa ni ongezeko la 7.1%. Serikali za mitaa toka vyanzo vya ndani shilingi bilioni 45.3.
Usafirishaji wa Bidhaa Nje : Mauzo ya nje yaliinza dola za kimarekani milioni 8,921 mwaka  2017  ikiwa ni pungufu kwa 3% ikilinganishwa na mwezi Machi, 2016.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo za hali ya uchumi, wala haihitaji kuwa na shahada ya uchumi kujua kama hali ya uchumi wa nchi yetu sio nzuri. Kwa mwenendo huo, ni dhahiri kuwa uchumi wetu unaporomoka na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza bunge hili juu ya mikakati iliyopanga ili kunusuru hali ya uchumi wetu ambayo kwa vigezo vyote inaporomoka.

HALI YA UCHUMI WA TAIFA  TAARIFA YA  BENKI YA DUNIA
Mheshimiwa Spika, Tarehe 11 Aprili, 2017 - Benki ya Dunia ilitoa Ripoti yake juu ya uchumi wa Tanzania na ilikuwa na haya ya kusema :
Kukua kwa uchumi kumepungua kutokana na upatikanaji wa fedha kuwa hafifu na kutotabirika/kutokueleweka  kwa Rais Magufuli.
Kuubadilika badilika kwa sera za serikali na ukuaji kwa kasi ndogo kwa sekta binafsi ilipunguza  ukuaji wa pato la ndani  toka 7.2% ( 2015)  mpaka 6.9% (2016)
Wawekezaji  wana wasiwasi/ mashaka na  sera zisizotabirika  kutoka za serikali ya Rais Magufuli.
Kuporomoka /kushuka kwa kasi kwa mzunguko wa fedha na kuongezeka kwa Mikopo isiyolipwa kumeiathiri sana sekta binafsi.
Kubadilika badilika kwa sera kunapotokea mara kwa mara kunasababisha sintofahamu  kwa sekta binafsi na sintofahamu husika zina athari katika maamuzi ya wawekezaji.
Mabenki ya Tanzania yanajilinda /yanajiwekea wigo Mkubwa (LARGE BUFFER) dhidi ya hasara inayopatikana kwa Mikopo isiyolipwa (kutokana na hali mbaya ya kibiashara tokea awamu ya tano iingie madarakani) kwa kutoza riba kubwa katika Mikopo.
Baadhi ya wawekezaji wa kigeni wameamua/ wanataka kupunguza  shughuli zao za uzalishaji  au  kusitisha mipango ya kupanua shughuli za uwekezaji kwa sababu ya masharti mapya magumu na kutozwa kodi kubwa. Tanzania inatajwa kuwa nchi ambayo sio rahisi  kufanya biashara ikiwa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya malipo (the highest number of payments) katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kuna malipo tofauti tofauti zaidi 48 ya kikodi.Na ni nchi ya pili  kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kodi (44.9%) katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Hii ndio taswira ya hali ya mwenendo wa uchumi wetu kutokana  na uchambuzi uliofanywa na wataalam wa fedha na uchumi  kitaifa  na kimataifa. Pamoja na yote hayo tunaambiwa kila kitu kinakwenda vyema!! Uongo huu na upotoshwaji unaofanya na serikali hii kupitia wizara ya fedha lazima ufike mwisho!!

MAENDELEO YA KISEKTA  SEKTA YA UZALISHAJI  VIWANDA

Mheshimiwa Spika, baada ya hotuba za wizara mbalimbali kukamilika tumegundua yafuatayo:
Kwamba, kwa mwaka wa fedha 16/17 serikali imeweza kutekeleza 30% tu ya miradi ya Maendeleo
Kilimo Kinachoajiri 75% ya watanzania kimezidi kudorora.. ukuaji umeporomoka mpaka 1.7 % toka 6% iliyotarajiwa
Viwanda vingi vilivyosajiliwa TIC ni viwanda ambavyo havina uhusiano wa moja kwa moja na shughuli pana za kiuchumi za nchi yetu.
 Viwanda vya usindikaji wa bidhaa zitokanazo na kilimo, Mifugo na uvuvi  sio kipaumbele cha serikali
Hakuna uhusiano  wa moja kwa moja kati ya sekta ya kilimo , sekta ya viwanda na nishati. Viwanda haviwezi kuwa imara bila kuwa ma malighafi za kutosha kutoka kwa wazalishaji na Umeme wa kuweza kuviendesha.
Hakuna dhamira ya serikali kufufua kilimo. Kijiografia Tanzania ilipaswa kuwa kapu  la nafaka la Afrika ya Mashariki na Kati , yenye uwezo wa kuzalisha  chakula kitakachotosheleza mahitaji ya ndani na zida kwa ajili ya nchi Jirani
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya waziri mkuu, ukurasa  wa 19 iliainisha kwamba  katika kuhakikisha  watanzania wanashiriki  kikamilifu  kwenye uchumi  wa viwanda , serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi  ya hapa  nchini Pamoja  na Mashirika  ya umma inajenga viwanda. Na kwamba jitihada hizo zimewezesha  Mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF, LAPF,LAPF,GEPF ,PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza  na kujenga   viwanda  vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini!
Mheshimiwa Spika, Taarifa  ya mwaka ya shughuli za Kamati nya kudumu  ya Bunge  ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC ) kwa kipindi  cha Januari  ,2016  hadi  Januari 2017 ikizungumzia madeni  makubwa  ambayo serikali inadaiwa na Mashirika  na Taasisi zake inaainisha kwamba  Kamati ilipokea  taarifa  ya msajili wa hazina kuhusu utendaji  wa taasisi mbalimbali za umma  na kubaini madeni  makubwa ambayo serikali inadaiwa  na Taaasisi hizo. Taarifa ya Kamati inasema. Kwa ujumla uchambuzi wa Kamati  umebaini kuwa  serikali imekuwa  na tabia ya kutumia huduma au kukopa  kutoka katika taasisi zake bila kufanya malipo. Serikali imekuwa ikidaiwa fedha nyingi  na madeni hayo yamekuwa yakilimbikizwa  mwaka hadi mwaka . Hali hii inadidimiza  ukuaji wa Taasisi hizo na kusababisha  hasara kuwa katika utendaji wao.
Mheshimiwa Spika, Mfuko ambao unaonekana kuathirika zaidi ni Mfuko wa PSPF ambao unaidai serikali zaidi  ya shilingi Trillion 3.3. ambayo yanajumuisha Madeni yanayotokana na dhima  ya mafao  ya watumishi  wa serikali ambao  walirithiwa  na mfuko wa PSPF kipindi iliyoanzishwa mwaka 1999 (pre 1999).
Mheshimiwa Spika, Mpaka kufikia Juni 2015, serikali ilikuwa inadaiwa shilingi trillion 1.97. Kiasi kilicholipwa na PSPF kwa wastaafu kimezaa riba ya shilingi bilioni 698 na kusababisha deni la shilingi trillion 2.67. Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa na Mfuko, uwezo wa mfuko kulipa kulipa mafao kwa wanachama wake  unategemeana na namna serikali itakavyolipa michango yake kwa wakati  pamoja na kulipa deni  la wanachama kipindi cha utumishi kabla ya julai 1999.
Mheshimiwa Spika, Kundi la pili linatokana na  madeni ya uwekezaji . Kumekuwa na kukinzana baina ya serikali na mfuko wa PSPF . wakati serikali  inadai deni inalodaiwa ni  bilioni 290 , mfuko wa PSPF  unadai deni halisi  ni shilingi   bilioni 533. Pamoja na mkanganyiko huo , serikali imeshindwa  kutekeleza ahadi yake   ya kutoa  hati fungani  zenye  thamani  ya shilingi  bilioni 290 kwa ajili ya kulipa deni hilo. Na deni la tatu  ni madeni ya malimbikizo  ya mchango wa mwajiri (15% ya serikali kila mwezi)  Deni linalotokana na malimbikizo ya shilingi bilioni 253.78 ambalo  ni la kipindi  cha kuanzia  Julai 2015 hadi Februari  2016.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inadaiwa  madeni makubwa  katika Mifuko mingine, miongoni mwao ni NSSF,LAPF , NHIF ,PPF  n.k  kama ambavyo taarifa za Kamati za Bunge na Taarifa za Mkaguzi Mkuu wa  Hesabu Serikali zinazotolewa kila mwaka zinavyoaainisha.. Kambi rasmi ya upinzani inashangazwa na kushtushwa na pendekezo hili jipya la kutumia Mifuko hii hii  kujenga viwanda  vipya 27, wakati serikali  hailipi madeni inayokopa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haiwezi kuruhusu wizi wa namna hii kuendelea kufanywa na Serikali dhidi ya fedha za wavuja jasho wa nchi hii! Ikumbukwe kwamba, hizi sio fedha za serikali, ni fedha za wanachama wanazochanga ili waweze kulipwa mafao punde wanapostaafu. Serikali inalazimisha mifuko kujenga viwanda wakati bado fedha za mifuko zilizotumika katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali (hususan sekta ya nyumba) zikiwa hazina uhakika wa kurejeshwa kutokana na maamuzi mabovu ya uwekezaji yaliyofanywa na Mashirika husika.
Mheshimiwa Spika, Ni muhimu sana hapa ikaeleweka kwamba , hatupingi Mifuko ya hifadhi kushirikiana na serikali katika uwekezaji,lakini ni uwendawazimu tukiendelea kuiruhusu serikali kuifanya Mifuko hii ni mirija ya kuchota fedha pasipo kulipa! Tunamtaka waziri wa fedha  aliambie Bunge hili tukufu:
 Katika Bajeti ya mwaka 2017/18 wametenga kiasi gani maalum kwa ajili ya kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii?
 Utaratibu wa utekelezaji wa malipo ukoje tofauti na makubaliano yaliyopita ambayo serikali haikuyatekeleza?
 Viwanda 27 vinavyotarajiwa kujengwa na fedha za mfuko kila mfuko utachangia kiasi gani na kwa utaratibu gani wa mrejesho wa fedha za wanachama?
Viwanda husika vitajengwa wapi? Na vigezo gani vimetumika katika uchaguzi wa maeneo ya kujenga viwanda husika?
Kama mradi wa viwanda tajwa unalipa, ni kwa nini sekta binafsi haijengi? badala yake zinatumika fedha za wanachama?

DENI LA TAIFA  (Fungu 22)
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa linasimamiwa  na Sheria  ya Madeni , Dhamama na Misaaada ya Serikali ya Mwaka 1974 ((iliyorekebishwa  2004) na kulingana na vifungu namba  3 na 6  vya sheria ya madeni , dhamana na misaaada ya serikali ,1974. Waziri wa  Fedha  ndiye mwenye dhamana ya kukopa na kutoa dhamana kwa niaba ya serikali.
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeendelea kuwa changamoto kubwa kwa uchumi wetu. Kukua kwa Deni la Taifa kunasababisha bajeti ya Serikali kuendelea kuwa tegemezi na hivyo kushindwa kutatua kero za kiuchumi za wananchi. Kwa bahati mbaya wananchi wengi hawaelewi undani wa deni la taifa na athari zake katika maisha yao ya kawaida. Jambo la kusikitisha ni kwamba Serikali imekuwa ikitumia mwanya wa wananchi kutokufahamu kwa undani athari za deni la taifa kuendelea kukopa mikopo mikubwa yenye masharti ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, Kuendelea kukopa Kwa namna hiyo kunaendelea kuwabebesha walipa kodi wa Tanzania mzigo mkubwa wa madeni ambayo yanazidi kufanya hali ya maisha kwa wananchi iendelee kuwa ngumu kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kulipa madeni badala ya kuzitumia fedha hizo kugharamia miradi ya maendeleo.

Mseto wa Deni la Taifa na Madhara yake Kibajeti
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Benki Kuu ya mwezi April, 2017 na Hotuba ya Bajeti 2017/18 inaonyesha kwamba Deni  la Taifa  limefikia  shilingi  trillion 50.8 (Ikumbukwe mpaka mwaka jana Juni 2016 deni la Taifa lilikuwa shilingi Trillion 41) .Deni la ndani likiwa  shilingi trillion 10.978. na deni la nje likiwa shilingi trillion 39.3 ( USD 17,578). Kwa kipindi cha mwaka mmoja deni la Taifa limeongezeka kwa  Dola za Kimarekani milioni 884.8 ( sawa na shilingi trilioni 2).
Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kwamba  kwa mwaka wa fedha 2016/17 kati ya  shilingi  8,671,038,922,510(Trillion 8.67) zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo (Wizara  ya Fedha) shilingi 8,009,341,187,000 (Trilion 8) zilikuwa ni kwa ajili ya kulipia deni la Taifa. Fedha zilizotumika kulipa deni,ni fedha nyingi kuliko  fedha zilizotumika kwa miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa deni la nje Serikali kuu peke yake  inadaiwa Dola za Kimarekani 13,792.9 (Tshs  Trillion 30.8). Kwa mwaka mmoja pekee nyongeza ya mkopo (deni la nje)  ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 455.4 ( Tshs Trillion 1. 018) Rejea Jedwali : External Debt Stock Borrowers katika Ripoti ya BOT ya Aprili, 2017.
Kwa upande wa Deni la Ndani:  Mpaka mwezi Mach, 2017 deni la ndani lilifika shilingi 10.976.8 bilioni. Ongezeko la mwezi la  shilingi  bilioni 327 na ongezeko la mwaka  kwa shilingi Trillion 1.53
Rejea Jedwali 5.1 :  Deni la Serikali (Government  Domestic Debt  Stock) 2007-2017 (Ripoti ya BOT mwezi April 2017)
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa deni la ndani wakopeshaji wakuu ni   Benki za biashara (41%) ,mpaka mwezi  Machi, 2017 wanaidai serikali  shilingi   4,578.8 bilioni (Trillion 4.578), wakifuatiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii,  (27%), ambayo mpaka Mwezi March  2017  wanaidai  serikali shilingi Trillion 2.995.3 , nyongeza ya shilingi Trillion 1.482 ukilinganisha na mwezi Machi, 2016.
Rejea Jedwali namba 5.4 (Ripoti ya BOT mwezi April 2017): Linaloonyesha mchanganuo wa deni  la ndani la serikali.

Mheshimiwa Spika, Imekuwa ni kauli za serikali kwamba deni la Taifa ni himilivu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tumekuwa tukitoa tahadhari ya mara kwa mara kutokana na ukweli kwamba serikali imekuwa ikihamisha goli (Change of Goal Post) kila mara ili kujitafutia uhalali wa kuendelea kukopa huku Taifa likiingizwa kwenye matatizo makubwa. Katika hotuba yetu ya mpango wa Taifa wa mwaka 2017/18 tulilihoji hili pasipo kupatiwa majibu.Cha kushangaza ni kwamba kauli za uhimilivu zimeanza kutajwa toka 2008 wakati deni likiwa shilingi Trilion 7.8  mpaka 2017 deni likiwa limefika shilingi Trillion 50.8
Mheshimiwa Spika, Baada ya hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni za kipindi kirefu (2010/11; 2011/12; 2012/13, 2013/14, 2014/15; 2015/16 na 2016/17) hatimaye tahadhari juu ya uhimilivu wa deni la Taifa imetolewa na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali. Katika Taarifa yake ya mwaka iliyotolewa mwezi Machi, 2017 Mkaguzi Mkuu alikuwa na haya ya kusema :
Deni la Taifa  lilianza kukua kwa kasi  tangu mwaka  2007/08 wakati nchi ilipopata msamaha wa madeni
Deni ya  Taifa limeongezeka kwa  149%  kwa miaka mitano iliyopita  bila kuhusisha madeni yaliyoachwa nje ya mseto
Mikopo isiyo ya masharti nafuu yanaongezeka  kwa 17% . Kutoka shilingi  bilioni  7,835 mwaka  2014/15 mpaka shilingi  bilioni 9.155  mwishoni  mwa mwaka 2015/16 . Na mikopo yenye masharti nafuu kupungua . Mwaka 2012 mikopo ya masharti nafuu  ilikuwa 89% ya deni la nje  ikilinganishwa na  69%  mwishoni mwa mwaka 2015/16. Hii ni kusema kwamba  mikopo isiyo ya masharti nafuu (Mikopo ya Kibiashara) ilikuwa 31% ya deni la nje  mnamo mwezi Juni 2016 ikilinganishwa  na 11%  miaka mitano iliyopita.
Ongezeko la madeni ya nje yenye masharti ya kibiashara unaongeza gharama za kuhudumia deni kadiri mikopo inavyoiva . Hii ni kutokana na vipindi vifupi  vinavyotolewa  katika kulipa deni ( mara nyingi miaka mitatu), riba kubwa  na muda mfupi wa deni kuiva!
 Taarifa ya uhimilivu wa deni la Taifa inaonyesha kwamba  kwa kuangalia gharama za kuhudumia  deni la Taifa ,ikilinganishwa  na mapato ya ndani ,gharama hizo ziko juu sana .Gharama  za kuhudumia  deni  zikichanganywa  na gharama  nyingine  kama vile  mishahara ya wafanyakazi ni gharama ambazo zinaiacha serikali na kiasi kidogo  sana cha fedha za kugharamia  miradi ya maendeleo  na huduma nyingine za kijamii.
Kutokana  na rasilimali  kuelekezwa  katika kulipa madeni , ni kiashiria  kuwa serikali  itaendelea kutegemea mikopo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Matokeo ya utegemezi huu ni kukua  kwa madeni ya ndani  na nje ambayo siyo  ya masharti nafuu. Mikopo husika pia inaendelea kuongeza gharama za kuhudumia deni.  ongezeko la mikopo isiyo ya masharti nafuu na mikopo ya ndani imesababisha gharama za kukopa kuwa juu, CAG  anatoa wito kwa watunga sera kuchukua tahadhari.

Serikali kukopa ndani kwa wingi kunasababisha msongamano  wa sekta binafsi katika fedha  chache zitakazokuwa zimebaki katika mabenki. Kwa lugha nyingine CAG anasema kukopa kwa wingi kwa serikali katika mabenki ya ndani kunaua uwezo wa wafanyabiashara wa ndani kukopa! hata wakifanikiwa kukopa masharti yanakuwa magumu sana.

Muundo na Usimamizi wa Deni la Taifa Kupitwa na Wakati
Mheshimiwa spika, Mkakati wa Taifa wa Madeni (NDS) wa mwaka 2002 uliandaliwa  kwa mazingira ya sheria ya Mikopo ya serikali , Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 (Miaka 43 iliyopita). Hali ya uchumi  na mazingira ya kuanzishwa  kwa sheria  na mkakati wa NDS yamebadilika  mno kutokana na mabadiliko ya kiuchumi ambayo yametokea.
Mheshimiwa Spika, Kutokana  na kupanuka  kwa wigo wa deni la Taifa  katika suala  la vipengele na mikopo mikubwa  ambayo imefanyika, sheria na miongozo inayosimamia  deni la Taifa haiko sambamba  na maendeleo hayo na vyombo vinavyotumika vimepitwa na wakati  na kwa sababu hiyo kufanya usimamizi wa deni la  taifa kuwa changamoto.
Mheshimiwa Spika, Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali anabainisha  katika ripoti yake aliyoitoa hivi karibuni kwamba wakati wa mahojiano na idara mbalimbali zinazosimamia deni la Taifa  chini ya wizara ya fedha ( idara ya uchambuzi wa sera (PAD), Mhasibu Mkuu wa Serikali (ACGEN), Idara ya fedha za Nje(EFD), Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango na Benki Kuu ya Tanzania amebainisha kwamba  mfumo uliopo sasa unaongeza uzembe katika uendeshaji,uratibu duni na  kutokuwa na taarifa za kutosha katika vitengo na taarifa sahihi  kupitia taasisi na kusababisha  kuwa na rekodi zisizosahihi  na  zisizojitosheleza  kuhusiana na deni !!haya ni maneno ya CAG !!!
Mheshimiwa Spika, katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia kati 6.5 na 7 kwa mwaka, ni vigumu sana kuweza kulipa deni la Taifa linalokua kwa 149% kwa miaka 5. Bila kuwa na vyanzo vipya vya mapato  au kusamehewa deni hili itakuwa vigumu sana kuweza kulipa deni hilo kikamilifu. Hii ni kwa sababu uwiano wa ukuaji wa uchumi hauendani na kasi ya ukuaji wa deni hata kidogo. Pamoja na upungufu wote huu, Serikali imeendelea kujitapa kuwa inakopesheka, na hivyo kuashiria kutokuwepo na hofu yeyote ya kukopa huku holela.
Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa  ya mikopo hii inakopwa katika soko la ndani. Hali hii imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa wananchi na wajasiriamali wanaotaka kukopa ili kukuza mitaji. Hali hii hufanya riba za mabenki kushindwa kushuka na hivyo kuwaathiri wakopaji na uchumi wa nchi kwa ujumla. Kwa maneno mengine, serikali imekuwa inazuia wajasiriamali wasikope kwa riba za bei nafuu, hivyo kufanya baadhi ya wanaokopa kwa riba zilizopo, ambazo ni kubwa kufilisiwa. Hali hii hurudisha biashara nyuma na inainyima serikali fursa ya kukuza uchumi na kukusanya mapato zaidi.

Mzigo Mkubwa wa Deni kwa Taifa (Debt Stress)
Mheshimiwa Spika, Matokeo ya uchambuzi  wa uhimilivu wa deni la Taifa  uliofanyika  mwaka 2015  na 2016  inaonyesha kuwa  uwiano wa gharama za kuhudumia deni na mapato ya  nchi (vyanzo vya ndani ya mapato) unakua kwa kasi sana . Hili limejidhihirisha katika bajeti ya mwaka 2016/17 ambapo serikali kupitia vyanzo vyake vya ndani (mapato ya kodi, mapato yasiyo na kodi na mapato ya serikali ya mtaa) ilifanikiwa kukusanya shilingi trillion 13.5. Fedha zilizotengwa kuhudumia deni la Taifa zikiwa shilingi 8,009,341,187,000 (Trilion 8). Na fedha zilizotengwa kwa ajili ya mishahara ni Trillion 7.2.
Mheshimiwa Spika,
 Mchanganuo hapo juu unatuonyesha kwamba Kwa mishahara na deni la Taifa peke yake fedha zilizotumika shilingi Trillion 15.2 huku makusanyo ya nchi yakiwa ni shilingi 13.5 Kwa tafsiri nyingine werikali ina uwezo wa kulipa mishahara na kuhudumia deni la Taifa tu! Huku ikiwa na upungufu wa shilingi Trillion 1.7. Bila mikopo serikali isingekuwa na ubavu wa kufanya shughuli yoyote ile!! Hii ni hatari
Mheshimiwa Spika, Hali kama hii inatarajiwa kujitokeza katika bajeti ya mwaka 2017/18 kwani kati ya shilingi Trillion 19 zinazotarajiwa kukusanywa kutokana na mapato ya Ndani , Shilingi trillion 16.6 zinatarajia kulipa misharaha na kuhudumia deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka huu sababu serikali imejiwekea maoteo makubwa ma makusanyo ambayo hayana uhalisia. Kama mwaka 2016/17 ilipanga kukusanya shilingi Trillion 29.53 ikaambulia kukusanya shilingi Trillion 20.7 (Pungufu ya Trillion 9) Ni miujiza gani itakayoiwezesha serikali kukusanya Trillion 31.7 kwa mwaka wa fedha 2017/18?!!

Serikali Inakopa kwa Masharti ya Kibiashara Kulipa Mikopo: Maajabu!!!!!
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri, inaonyesha kwamba  serikali inatarajia kukopa shilingi Trillion 7.763 kutoka soko la ndani  na nje kwa masharti ya Kiabiashara. Mikopo ya ndani  ikiwa shilingi  Trillion 6.168, ambapo  shilingi  bilioni 4.948.2 ni kwa ajili ya kulipia  dhamana za serikali zinazoiva.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa aina hii unachangia kwa kiasi kikubwa  kuongeza mzigo wa deni kwa nchi!  Serikali imeshindwa kulipa madeni kwa kutumiavyanzo vyake vya mapato!

Tabia hii inazidi kuota mizizi, kwani katika mwaka 2014/15 kati shilingi trilioni 1.8 zilizokopwa katika soko la ndani, zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zilitumika kulipa madeni ya hati fungani wakati shilingi trilioni 0.69 tu ziliwekwa kwenye miradi ya maendeleo. Hiki ni kiashiria cha karibu sana kwa serikali kufilisika.
Mheshimiwa Spika, Kukopa mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa ili kulipa mikopo yenye riba ndogo au kwa uendeshaji wa kawaida wa serikali au taasisi zake ni kiashiria cha kutosha kuainisha maamuzi yasiyo na uelewa wa kawaida sana wa utawala na usimamizi wa fedha. (basic business and economic sense). Mikopo ya kibiashara hutafutwa kwa matumizi ya uwekezaji wenye lengo la uzalishaji.

Imani ya Taasisi za Fedha za Kimataifa kwa Tanzania Imepungua
Mheshimiwa Spika, Imefikia hatua hata  kupata hiyo mikopo ya biashara  imekuwa shida. Katika bajeti ya mwaka 2016/17 serikali ilipanga kukopa kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara  shilingi trillion 2.1 ili kugharamia miradi ya maendeleo. Fedha hizo hazikupatikana kwa maelezo kwamba  soko la fedha za kimataifa kutokuwa na hali nzuri.
Mheshimiwa Spika, sababu inayotolewa na serikali haina ukweli. Ukweli ni kwamba taasisi za fedha za kimataifa zinakwepa kuikopesha serikali kwa sababu haina uhakika  juu ya uwezo wa serikali wa kulipa mkopo pamoja  riba kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imekuwa ikikwepa kufanyiwa tathmini/uhakiki wa uwezo wa kukopesheka (Credit Rating) kwa kipindi kirefu sasa,inashindwa hata na Rwanda!! sijui kuna siri gani inafichwa. Matokeo yake wanatarajia kupewa mikopo kwa huruma na hisani jambo ambalo halifanyika katika ulimwengu wa Biashara!
Mheshimiwa Spika, Ili kuweza kutanzua kutendawili na utata wa deni hili;
 Ni rai ya kambi rasmi ya  upinzani bungeni kurudia ushauri tulioutoa miaka minne na kulitaka Bunge liridhie na kumwelekeza Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kufanya ukaguzi maalum (special audit) katika kitengo cha Deni la Taifa (fungu 22) ili kujua mikopo inayochukuliwa kila wakati inatumika kufanyia nini, na miradi iliyotekelezwa kama ni miradi ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kuitaka serikali kama ambavyo tumesema miaka mitano iliyopita kulitaka  Bunge  litunge sheria  ili liweze  kudhibiti ukopaji na matumizi ya mikopo ya serikali. Vile vile tunapendekeza katika sheria hiyo iwe lazima kwa serikali kupata kibali kutoka katika Bunge  kabla ya kuweza kukopa. Hii inafanyika katika nchi nyingi  duniani kama vile Marekani na Uingereza.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali wakati wa majadiliano ya mikataba ya mikopo, kutumia utaratibu wa Interest rate swapkutokana na ukweli kwamba sababu mojawapo inayosababisha deni kukua kwa kasi kunatokana ni kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu  na kuwa na riba ambazo zinabadilika mara kwa mara. Interest swapping maana yake ni kukubaliana kuweka kiwango cha riba kulingana na thamani ya shilingi ambayo inasaidia kuwa ni kiwango kilekile cha riba bila kujali kama thamani ya  shilingi itapungua  au itaongezeka. Hii inasaidia kufanya deni lisiongezeke kwa kasi kutokana na kupungua kwa thamani ya shilingi.
Mheshimiwa Spika, Ukirejea uchambuzi tulioufanya hapo juu kuhusiana na deni la Taifa na tishio lake katika mustakabali wa nchi hii, ni mwendawazimu pekee ambaye hataona hatari kubwa sana iliyo mbele yetu. Ni lazima sasa Bunge lako tukufu lichukue nafasi yake kuisimamia serikali kiukamilifu kama matakwa ya katiba yanavyolitaka ili kulinusuru Taifa.


UPOTEVU WA MAPATO KATIKA SEKTA YA MADINI NA HADITHI ZA MCHANGA ZA SERIKALI YA CCM
Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni kumeibuka mjadala mpana juu ya rasilimali za nchi yetu baada ya sakata la Makinikia ama Mchanga wa Dhahabu.Katika hali ya kushangaza kuna upotoshwaji wa makusudi unaotaka kufanywa wenye dhamira ya kuonyesha kwamba ETI LEO kambi Rasmi ya upinzani Bungeni inapinga MAMBO ambayo kwa miaka mingi huko nyuma tumekuwa tukiyapambania dhamira ikiwa utajiri wa nchi hii uwanufaishe watanzania .
Mheshimiwa Spika,Nirejee hotuba yetu ya miaka ya karibuni  iliyosomwa na aliyekuwa waziri kivuli wa fedha na Uchumi  Ndugu James Fransis Mbatia wakati akiwasilisha HOTUBA MBADALA ya Bajeti  mwaka 2014/15  akiielezea serikali ya CCM juu ya upotevu wa MAPATO katika sekta ya Madini.  Naomba nirejee maelezo yake kama ifuatavyo:
Taarifa za shirika la fedha Duniana (International Monetary Fund - IMF) zinabainisha kuwa kati ya mwaka (2008  2011) mapato ghafi ya dhahabu yaliongezeka toka Dola za Marekani millioni 500 hadi bilioni 1.5  kwa sababu ya kuongezeka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu kuongezeka dhamani,  lakini mapato kwa serikali yalibaki kuwa  Dola za Marekani  milioni 100 kwa mwaka kwa wastani.Hali hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa kwa msamaha wa kodi kwa makampuni (Corporate income tax holidays). Hakuna kampuni hata moja liliyolipa kodi hii hadi 2012. Taarifa ya IMF inaonesha pia kwa kuzingatia hali hii, hakuna mategemeo kuwa kipato kutokana na madini kitaongezeka hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupitishwa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010, migodi iliyopo bado inaendelea kulindwa na mikataba iliyoingiwa kwa kutumia sheria iliyofutwa. Makubaliano ya kati ya Serikali na makapuni hayo inaonesha kuwa Tanzania inapoteza fedha nyingi sana, kwa mifano:

Taarifa ya Tume ya Bomani ilikadiria serikali ilipoteza  sh. bilioni 39.8  mwaka 2006/7 na sh. bilioni 59 mwaka  2007/8 kutokana na msamaha wa kodi ya mafuta tu (fuel levy exemptions)  kwa makampuni sita tu. Kufikia mwishoni mwa mwaka 2011, makampuni ya uchimbaji madini yalikuwa yanadai takribani Dola za Marekani miioni  274 kurejeshewa kutokana na msamaha wa kodi hiyo toka 2002.

Makampuni yamepewa haki ya kumiliki  madini yake, ikiwemo haki ya kuuza hisa na mitaji yake bila kulipa kodi ya mapato (capital gains tax).

Mikataba na sheria inawapa makampuni ruksa ya kutumia hasara wanazopata kufidia kulipa kodi.

Mwaka 2010, Tanzania Minerals Audit Agency (TMAA) ilikagua makampuni 12 na kugundua mapungufu/udanganyifu wa matumizi ya makampuni wa  Dola za Marekani milioni 705.8, ambapo serikali ilikosa  mapato ya Dola za Marekani 176 milioni. Hii ilikuwa mara ya kwanza TMAA kufanya ukaguzi, je, kwa miaka 10 kabla ya hapo serikali ilipoteza kiasi gani cha mapato?

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Viongozi wa Kidini juu ya Haki za kiuchumi na Umoja (A report commissioned by the Interfaith Standing Committee on Economic Justice and the Integrity of Creation) iliyoitwa The One Billion Dollar Question iliyotokana na utafiti wa kutafuta mianya na kiasi cha upotevu wa mapato kwa nchi katika sekta ya madini, upotevu wa mapato ulikadiriwa kufikia  Dola za Marekani bilioni 1.07  kwa mwaka 2009/10 kwa njia ya misamaha ya kodi, ukwepaji kodi, uhamilishaji mitaji na vivutio vya kodi kwa uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, upotevu huo wa  Dola za Marekani bilioni 1.07  (takribani sh trilioni 1.7) ilikuwa ni takribani  asilimia 17  ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka 2009/10.  Hoja hizo zote za kambi zilijibiwa kwa kejeli kubwa sana na wabunge walio wengi wa CCM zikiongezewa mbwembwe na mtoa hoja (WAZIRI mwenye dhamana ya Fedha) , Rais Magufuli akiwa sehemu yao!

Mheshimiwa Spika, Tukiwa mwaka wa pili wa utekelezaji wa bajeti ya serikali ya awamu ya tano ya CCM , bajeti  ambayo imevunja rekodi kwa kuwa utekelezaji mbovu kuliko uliowahi kutokea kwa upande wa miradi ya maendeleo  (0-30%),Huku Halmashauri zetu zikiwa HOI BIN TAABAN kwa kunyanganywa mapato,  imeibuka hoja ya MCHANGA  WA DHAHABU. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  haihitaji Bunge lako tukufu kutumia misuli mingi kujadili mchanga ambao kwa mikataba yetu NI MALI YA MWEKEZAJI.  Mchanga ambao hata kama wote ungegeuka dhahabu leo ,stahili yetu kama nchi ni  mrabaha wa asilimia nne tu!! Tunataka Bunge lijadili kuhusu DHAHABU yetu na madini yetu mengine yanayoibiwa kila uchwao NA SIO MCHANGA!
Mheshimiwa Spika, Tunataka Bunge hili lirejee makosa yaliyofanywa na wana CCM  wenzao mwaka 1997(KUJISAHIHISHA na kuwaomba Radhi watanzania)  walipoleta sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali  za fedha ( Financial Laws Miscellaneous Amendments Act 1997) ambayo ilifanya marekebisho makubwa katika sheria mbalimbali za kodi , tozo na ushuru mbalimbali kwa makampuni ya madini. Matokeo yaliyoisababishia nchi  kukosa mapato  ya kutosha  katika madini, matokeo yake nchi inashindwa kujitosheleza kibajeti ,inajiendesha kwa kukopa huko huko kwa wanufaika wa MADINI yetu na sasa deni la TAIFA limefikia shilingi Trillion 50.8
Mheshimiwa Spika, Tukifika hapo, TUTAMPOGEZA RAIS, lakini si kwa maigizo yanayofanyika sasa.

WANANCHI WANATAKA BAJETI INAYOZINGATIA UKUAJI SHIRIKISHI  INCLUSIVE GROWTH
Mheshimiwa Spika, Hakuna ubishi kwamba mipango mbali mbali ya serikali imekuwa ikigonga mwamba kwa sababu mipango inakuwa mingi, fedha kidogo na hakuna mwendelezo (consistency). Jambo likipangwa kutekelezwa kwa miaka mitano , lisipofanikiwa tunarukia jambo lingine hata kama hatukufanya uwekezaji wakutosha, Matokeo yake hakuna kinachofanikiwa!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kwamba huwezi kuondoa umasikini  bila kuigusa sekta inayoajiri watanzania walio wengi! TUNARUDIA Kama Kilimo hakitaendelezwa, ina maana kwamba, itakuwa ni ndoto kuondoa 75% ya  Wananchi wetu katika lindi la umasikini. Sekta ya Kilimo imedumaa si kwa sababu nyingine yeyote zaidi ya Ukweli kwamba hakuna uwekezaji wa maana unaofanyika!
Mheshimiwa Spika, Ripoti zinaonyesha kwamba Shughuli za kiuchumi za kilimo zilikuwa kwa kasi ndogo ya asilimia 3.5 mwaka 2014/15 ikilinganishwa  na asilimia 2.3 mwaka 2025/16 .Mwaka 2017 kimezidi kudidimia  kufikia 1.7%...tusishangae mwaka 2018 tukiambiwa ukuaji wa sekta hii imefikia 0.5%!! ni wazi kwamba hakuna miugiza inayoweza fanyika kama serikali inatenga shilingi bilioni 3.3 kuhudumia watanzania milioni 30 , wakati huo huo  shilingi Trillion 1 zimelipwa CASH kununua ndege ambazo zinahudumia watanzania 10,000.
Mheshimiwa Spika, Licha ya  kupuuzwa, bado sekta hii imeendelea kuongoza kwa kuwa na mchango mkubwa  katika pato la Taifa  kwa kuchangia kwa asilimia 29.0 ya pato la Taifa ikifuatiwa  na shughuli za ujenzi (13%), biashara na matengenezo (10.7%) na ulinzi na utawala 6.4%.
Mheshimiwa Spika, hata hotuba wa waziri I naonyesha ni kwa namna gani serikali ya CCM haina mpango kabisa na wakulima wan chi hii (75% ya watanzania) kwa miradi inayopewa msukumo wa KIPEKEE kwa mwaka 2016/17-2020/21 kati ya vipaumbele 8, suala la KILIMO limezungumziwa katika kamradi kamoja ka uanzishwaji wa shamba la miwa  nakiwanda cha sukari,na pesa zilizotengwa ni shilingi bilioni mbili tu!! HII NI ZAIDI YA MZAHA!
Mheshimiwa Spika,
ILI Kilimo kiweze kupiga hatua:-
Lazima tufanye utambuzi wa maeneo ya kipaumbele kwa Taifa
Utambuzi wa  aina  ya mazao ambayo ni kipaumbele kwa Taifa  baada ya  kufanya utafiti wa kina wa kujua   mahitaji ya soko; soko la ndani, kwenye ukanda wa Africa Mashariki, Afrika na Dunia ambayo yakifanyiwa uwekezaji maalum na ya kimkakati wa serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wakulima wadogo tutataweza ongeza pato la Taifa  na kupunguza umasikini lakini kubwa zaidi kusaidia ukuaji wa sekta nyingine!
Lazima kuwe na mkakati maalum wa kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati ( Maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati)
Miundombinu bora ya kuunganisha maeneo ya kimkakati na soko
Ujenzi na Upanuzi wa mabwawa ya umwagiliaji (irrigation schemes) kwenye maeneo ya mkakati
Hakikisha kuna pembembejeo za kilimo za kutosha sambamba na mbolea na mbegu k

No comments:

Post a Comment