Naibu Meya Viola Lazaro Akieleza kwa hisia kali alivyokamatwa na jeshi la Polisi. |
Madiwani hao wanaotokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Happy Chale na Sabina Peter walikamatwa jana wakiwa kwenye ofisi ya Meya wa jiji iliyopo kwenye makao makuu ya halmashauri hiyo.
Tukio hili limekuja siku chache baada ya Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji Meya wa Ubungo, Bonifasi Jacob na Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Hai, Helga Mchovu na kuwahoji ambapo wote hao wanatokana na chama cha CHADEMA.
Meya wa jiji, Calist Lazaro alithibitisha kuwa madiwani hao walikamatwa majira ya saa 9 alasiri ambapo alidai kuwa wanashikiliwa polisi kwenye kitengo cha uchunguzi wa makosa ya kimtandao ingawa hakujua sababu za kushikiliwa kwa !madiwani hao.
"Mheshimiwa Viola alikamatwa ofisini kwake (Ofisi ya Mstahiki Meya) akiwa anatekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi, waliokamatwa wengine ni Sabina Peter, Happiness Elia Chale ( Madiwani Viti Maalum) ambao wote walikuwa pamoja kwenye Ofisi ya Mstahiki Meya," alisema Meya Lazaro na kuongeza.
Sababu za kushikiliwa kwao bado hazijajulikana wazi lakini kwa sasa wanachukuliwa maelezo kwenye kitengo cha Cyber, Polisi Mkoa wa Arusha,".
WAELEZA WALIVYOKAMATWA
Diwani Sabina alisema kuwa hawajui wanashikiliwa kwa kosa gani ambapo alielezea namna walivyokamatwa.
Alisema kuwa yeye na diwani, Happy walikuwa wamefika ofisini hapo kufanya mazungumzo na Naibu Meya, Viola kisha waelekee kutoa pole kwenye msiba kwenye kata ya Ngarenaro.
"Tukiwa tunajiandaa kuondoka wakaingia polisi watatu wawili wa kiume mmoja wa kike, wakatuambia wanamuhitaji Naibu Meya, Viola hakubisha akasimama kwa ajili ya kuitikia wito huo akanipa pochi yake," alisema diwani Sabina na kuongeza.
Polisi wakasema wanamuhitaji aende na pochi yake pamoja na simu yake, nikarudisha pochi ya Naibu Meya wakaniuliza simu yake iko wapi nikawaambia sijui nikawaonyesha simu zangu mbili basi wakaniambia na mimi niko chini ya ulinzi,'.
Diwani, Sabina alisema kuwa baada ya polisi kusema wanamuhitaji Naibu Meya kwa ajili ya mahojiani diwani, Happy aliamua kuondoka ambapo polisi walimpigia simu kumuita baada ya kuikosa simu ya Naibu Meya.
"Mheshimiwa Happy yeye alikuwa kashaondoka, aliitwa na polisi waliotumia simu yangu kumpigia baada ya kuona hawaoni simu ya Naibu Meya wakasema sisi tumeipoteza makusudi ndiyo tuko hapa mheshimiwa Happy anaandika maelezo," alisema diwani, Sabina.
Hata hivyo juhudi za kumpata kamanda wa Polisi mkoani hapa, (RPC), Charles Mkumbo kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita muda wote bila kupokelewa.
0 Comments:
Post a Comment