Meli za Kivita za Marekani |
Kwa mara nyingine serikali ya Korea Kaskazini imeitahadharisha Marekani kwamba, ikiwa meli za kivita za nchi hiyo zitaendelea kuwepo katika Peninsula ya Korea, basi itaziangamiza silaha za nyuklia za Washington na kuzigeuka kuwa vyuma chakavu.
Taarifa iliyotolewa na Pyongyang sambamba na kuionya nyambizi ya nyuklia ya Marekani inayoitwa 'USS Michigan' iliyotumwa na Washington kwa kile ilichokidai kuwa ni kwa ajili ya kuzuia kuenea silaha za maangamizi katika eneo hilo, imesema kuwa ikiwa meli hiyo itaendelea kuwepo eneo hilo, basi haitasita kuizamisha. Imeongeza kuwa, kuendelea kukaribia nyambizi hiyo katika maji ya Korea Kaskazini, kutaifanya kukumbwa na hatari ya kuangamizwa.
Inafaa kuashiria kuwa, nyambizi ya nyuklia ya Marekani ya 'USS Michigan' iliwasili Korea Kusini wiki iliyopita kwa ajili ya kushiriki maneva ya kijeshi yanayoendelea baina ya Washington na Seoul. Kabla ya hapo pia, Marekani ilituma meli tatu za kubeba ndege za kivita katika maji ya Korea Kusini ambapo Pyongyang ilitangaza wazi kwamba, zana hizo 'dhaifu' za kijeshi za Marekani mkabala na nguvu kubwa ya kijeshi ya Korea Kaskazini, zitageuzwa na kuwa chuma chakavu. Siasa za uhasama za Marekani kuilenga Korea Kaskazini, zimeifanya Peninsula ya Korea kukumbwa na mvutano mkubwa.
Marekani inataka kuilazimisha Korea Kaskazini kusitisha miradi yake ya nyuklia na makombora ya balestiki, huku nchi hiyo ya Asia kwa mara kadhaa ikisisitiza kwamba maadamu Washington na washirika wake, hususan Korea Kusini na Japan zitaendeleza siasa za vitisho dhidi yake, basi nayo itaendelea kujiimarisha kijeshi kwa ajili ya kuzuia shambulizi lolote la adui dhidi yake.
No comments:
Post a Comment