Friday, May 12, 2017

IRAN , Leo Irana inaadhimisha siku ya kuzaliwa Mwokozi wa Ulimwengu Imam Mahdi AS.

Maeneo tofauti ya Iran ya Kiislamu hususan katika miji mitakatifu ya Mash'had na Qum jana ilighariki katika furaha za maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu, Imam Mahdi AS.
Kwa mujibu wa riwaya mbalimbali, leo Ijumaa mwezi 15 Shaaban 1438 Hijria inasadifiana na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS aliyeahidiwa na Bwana Mtume Muhammad SAW kudhihiri katika zama za mwisho za dunia na kuujaza ulimwengu haki na uadilifu.
Hapa nchini Iran, wapenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Ahlul Bayt AS na Imam Mahdi AS wameadhimisha siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huku msikiti wa Jamkaran wa mjini Qum, (kusini mwa Tehran) ukiwa umefurika Waislamu kutoka kona mbalimbali za dunia wakiwa na shauku kubwa ya kuona mwokozi huyo wa dunia anadhihiri haraka. 
Waislamu wa Iran wakiwa katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam Mahdi AS

Kwa kawaida, katika siku ya maadhimisho ya kuzaliwa Imam Mahdi AS, Waislamu wa Iran hukusanyika kwenye maeneo matakatifu, misikitini na hata mitaani kufanya sherehe mbalimbali na hasa kuomba dua na kusoma kasida zinazohusiana na mtukufu huyo.
Kwa mujibu wa riwaya nyingi, Imam Mahdi AS, mwana wa Imam Hasan al Askari AS alizaliwa mjini Samarrah Iraq mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria. Baba wa mtukufu huyo yaani Imam Hasan al Askari AS ni Imam wa 11 wa Waislamu wa Kishia.
Kuzaliwa mtukufu huyo kulitokea kwa siri, na watu wengi hawakuweza kujua kuzaliwa kwake isipokuwa wafuasi waaminifu wa Imam Hasan al Askari AS kutokana na ukandamizaji mkubwa wa watawala wa wakati huo, ambao waliweka ulinzi mkali nyumbani kwa mtukufu huyo ili kujaribu kuzuia kuzaliwa Imam Mahdi AS. Hata hivyo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alizaliwa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake. 
Riporti ya ParsToday

No comments:

Post a Comment