Kwa mara nyingine tena, Aprili 22, mwaka huu Tanzania imeshuhudia shambulio kubwa dhidi ya uhuru wa kukusanyika, kutoa maoni, uhuru wa habari na wanahabari baada ya watu waliokuwa wameficha sura zao 'kininja' wakiwa na silaha za moto, mapanga na marungu, kuvamia mkutano halali wa Viongozi wa CUF Wilaya ya Kinondoni wakiongozwa na Mwenyekiti Juma Nkumbi na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Hoteli ya Vina, Mabibo jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo viongozi hao wa CUF walishambuliwa, kujeruhiwa na mkutano huo kuvunjika.
Aidha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari, walioitikia wito wa kuhudhuria mkutano huo kama sehemu ya wajibu wao wa kitaaluma na kikazi, walishambuliwa, kutishiwa kuuwawa, kujeruhiwa, kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na kuzuiwa kutekeleza wajibu wao.
Tumelichukulia tukio hilo la jana kama shambulio na tishio jingine kubwa dhidi ya uhuru wa maoni, uhuru wa habari na wanahabari, ikiwa ni mfululizo wa matukio ya aina hiyo nchini ambayo yamekuwa yakitokea bila hatua stahili za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Taarifa za awali tulizozipata kuhusu tukio hilo mbali ya kuhusisha kuwa limefanywa na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba pia zimedai kuwa baadhi ya wahusika ni watumishi wa vyombo vya dola.
Mbali ya madai hayo, taarifa hizo zimehusisha kuwa tukio la jana lina uhusiano mkubwa ama wa kiuratibu au mkakati wa utekelezaji na matukio mengine ya namna hiyo kwa siku za hivi karibuni hasa tukio la kutishiwa bastola na kuzuiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa, Nape Nnauye na pia tukio la kuvamiwa kwa kituo cha matangazo cha Clouds Tv na Fm na watu waliokuwa na silaha za moto wakiwa wamevaa sare za askari.
Ni jambo la kusikitisha kwamba mgogoro uliopandikizwa na dola ukilelewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa kile kinachoonekana kuwa ni kwa manufaa ya CCM, sasa umefikia hatua mbaya ya kushambulia waandishi wa habari kwa silaha za moto (bastola), mapanga na marungu kisha kuwaumiza vibaya, kuharibu vifaa vyao na kutishia maisha yao mchana kweupe.
Tukio hilo la jaba ni dhahiri limezidi kutonesha vidonda vya wadau wa habari na Watanzania wote kwa ujumla na kuwakumbusha mfululizo wa matukio ya namna hiyo, Serikali ikishindwa kuchukua hatua zozote zile huku kukiwa na tuhuma za baadhi ya wahusika kuwa ni watumishi wa umma wa Watanzania katika vyombo vya dola.
Pamoja na tukio hilo kuwaathiri waandishi na vyombo vya habari vyote vilivyoitikia mwaliko halali wa viongozi wa CUF, waandishi wafuatao wameumia na hata wengine kuharibiwa vifaa vyao vya kazi.
1. Henry Mwang'onde (The Guardian) ambaye aliponea chupuchupu kudondoka kutoka ghorofa ya nne ya jengo la hoteli hiyo akijaribu kujiokoa dhidi ya wavamizi hao waliokuwa na silaha.
2. Mary Geofrey (Nipashe) ambaye ameshonwa kutokana na kupata majeraha mkononi wakati akijaribu kujiokoa dhidi ya wavamizi hao.
3. Kalunde Jamal (Mwananchi)
4. Rachel Chizoza (Clouds Tv na Fm)
5. Mariam Mziwanda (Uhuru)
6. Freddy Mwanjala (Channel ten) ambaye mbali ya kuumia pia amevunjiwa kamera.
7. Hamphrey Shayo (Michuzi Blog).
8. Aziz Kindamba wa Clouds Tv na FM ambaye ameumia na vifaa vya kazi kuharibiwa.
Ni jambo la kusikitisha kuwa tukio hilo la jana, limetokea ndani ya muda mfupi tangu tukio jingine la namna hiyo lilipotokea Kituo cha Clouds Tv na Clouds FM ambako watu wenye silaha za moto walivamia usiku.
Bila shaka wafuasi hao wa Prof. Lipumba wamepata kiburi na ujasiri wa kufanya ujahili huo baada ya kuona kuwa wavamizi waliovamia Clouds Tv na CLouds Fm pamoja kutambulika kupitia picha za video, hawajachukuliwa hatua zozote kwa kosa hilo kubwa la kijinai.
Halikadhalika wameona inawezekana kufanya tukio hilo kwa sababu watu waliomvamia, kumtolea bastola Nape na kumzuia asifanye mkutano na waandishi wa habari, hawajachukuliwa hatua yoyote pamoja na kujulikana kwa sura zao.
Kupitia taarifa hii, CHADEMA inalaani vikali tukio hilo la jana ambalo kama tulivyosema hapo juu, ni shambulio na tishio kubwa dhidi ya uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa habari na wanahabari nchini.
Tunatoa wito kwa wananchi wote na makundi mbalimbali ya kijamii, zikiwemo taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kupaza sauti na kulaani vikali matukio hayo na kuungana pamoja kudai uwajibikaji utakaorejesha imani na matumaini ya Watanzania ambao sasa wako katika sintofahamu kubwa ya namna nchi yao inavyotawaliwa.
Tunazitaka mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi wa kina na haraka kuwabaini na kuwachukulia hatua stahiki, ikiwemo kuwafikisha mbele ya sheria wote waliohusika kupanga na kutekeleza tukio la jana na mengine ya namna hiyo (kama tulivyoyataja) ya uvamizi, kujeruhi watu, kuwazuia kufanya kazi, kutishia kuua na kuharibu vifaa vyao vya kazi.
Tunawataka Msajili wa Vyama vya Siasa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nc
No comments:
Post a Comment