Thursday, April 3, 2014

Ikulu yachachamaa

Haya ndio Maelezo ya Ikulu kumjibu Warioba
na Gazeti la Raia Mwema la Leo Jtano. Soma
Kisha tujadiliane.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ufafanuzi kuhusu Tume ya Katiba
kutupiwa virago
Gazeti la Raia Mwema lililotoka leo,
Jumanne, Aprili 2, 2014, limeandika habari
zisizokuwa za kweli chini ya kichwa cha
habari : “Warioba: Ikulu imetutupia
virago”.
Habari hiyo inamkariri aliyekuwa Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akidai kuwa
Tume yake ilifukuzwa kazi, kwamba
haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha
nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka na
kwamba wajumbe wa Tume hiyo waliporwa
magari ambayo yamewekwa Ikulu.
Aidha, Gazeti la Mtanzania la leo pia,
limeandika habari, zisizokuwa za kweli vile
vile, chini ya kichwa cha habari: “Bilioni 6
kuipoza Tume ya Warioba”.
Habari hiyo inamkariri mjumbe mmoja wa
Tume hiyo, ambaye Gazeti halimtaji jina,
akidai kuwa Tume hiyo inatarajiwa kupewa
kiasi cha Sh.bilioni sita ikiwa ni kiinua
mgongo ambako kila mjumbe atapata kiasi
cha Sh. milioni mia mbili.
Habari zote mbili ni za uongo na Ikulu
inapenda kutoa ufafanuzi kama
ifuatavyo :
(a) Tume kufukuzwa kazi
Itakumbukwa kuwa moja ya mijadala mikali
ya awali kuhusiana na mchakato wa Katiba
Mpya ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imalize muda wake; wengine wakitaka
Tume imalize muda wake baada ya kukabidhi
Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba, wengine
wakitaka Tume imalize muda wake baada ya
Mwenyekiti wake Jaji Warioba kuwasilisha
Rasimu yake Bungeni na hata wengine
wakitaka wajumbe wa Tume wawe sehemu ya
Bunge Maalum la Katiba.
Hatimaye, ilikubaliwa kuwa Shughuli za Tume
zingefikia ukomo wake baada ya Mwenyekiti
wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye
Bunge Maalum la Katiba kama inavyoelekezwa
katika Kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba.
Kifungu hicho kinasema kuwa baada ya
kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba kwenye
Bunge Maalum chini ya Kifungu cha 20(3)
(cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba) Rais, kwa
Amri itakayochapishwa katika Gazeti la
Serikali, atavunja Tume.
Mheshimiwa Warioba aliwasilisha Rasimu ya
Katiba katika Bunge Maalum la Katiba
Jumanne ya Machi 18, mwaka huu, 2014 na
siku iliyofuata Jumatano, Machi 19, 2014 na
kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Rais alitia saini tangazo la Serikali la
Kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tangazo hilo lilichapishwa katika toleo
lililofuata la Gazeti la Serikali la Ijumaa,
Machi 21, 2014. Gazeti la Serikali
huchapishwa kila Ijumaa ya kila wiki.
Hivyo, tokea mwanzo wa mchakato mzima wa
Katiba Mpya na utendaji kazi wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba hapakupata kuwepo,
hata wakati mmoja, shaka kuhusu siku ya
Tume hiyo kumaliza kazi zake. Mwenyekiti wa
Tume, wajumbe wote wa Tume, Sekretarieti
ya Tume na Watanzania wote waliijua fika
siku ya mwisho ya Tume kukamilisha shughuli
zake. Kwa mtu kujitia ameisahau siku hiyo leo
ni kiwango cha juu sana cha unafiki.
Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu
haikuwa na madaraka wala mamlaka yoyote
kubadilisha tarehe hiyo. Hivyo, madai ya
Ikulu kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya
Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la
kutunga tu.
(b) Muda wa kuandaa na kukabidhi
nyaraka na ofisi
Hili nalo ni jambo la kutunga na kuzusha tu.
Mheshimiwa Jaji Warioba alikabidhi rasmi
Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais
wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein, Jumatatu ya Desemba 30, 2014, mbele
ya wananchi viwanja vya Ukumbi wa
Karimjee, Dar Es Salaam.
Hivyo, tokea siku hiyo, Tume haikuwa tena na
kazi ya kuandaa Ripoti ama Rasimu kwa
sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha na wala
isingeweza kuibadili tena Rasimu ya Katiba.
Kwa maana hiyo, tokea Desemba 30, mwaka
jana, kupitia miezi ya Januari, Februari mpaka
Machi 18, mwaka huu, Sekretariati ilikuwa na
muda wa siku 77, zaidi ya miezi unusu,
kufanya maandalizi ya kukabidhi nyaraka na
ofisi kwa sababu ilijua kazi yake ilikuwa
inamalizika siku ambayo Mwenyekiti wa Tume
hiyo angewasilisha Rasimu ya Katiba katika
Bunge Maalum la Katiba.
Sasa katika muda wote huo, Sekretarieti ya
Tume ilikuwa inafanya nini badala ya kuandaa
ripoti ya makabidhiano na wakati maofisa
wake walikuwa wanaendelea kulipwa
mshahara na Serikali? Kwa nini walalamike
hadharani leo kwa jambo ambalo lilikuwa ni
la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa
wakati?
(c) Wajumbe wa Tume kutakiwa
kurudisha magari Ikulu
Ni kweli kuwa wajumbe wa Tume walitakiwa
kurudisha Ikulu magari ambayo walikuwa
wanatumia kikazi kwa sababu kazi ya Tume
ilikuwa imemalizika.
Pili, Tume ilijua tokea mwanzo kuwa baada ya
kumaliza kazi yao, magari ambayo walikuwa
wanatumia wajumbe na maofisa wa Tume
hiyo yalikuwa yanatakiwa kupelekwa Dodoma
kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalum
la Katiba ambalo linakabiliwa na shida kubwa
ya usafiri.
Serikali ilichukua uamuzi kuwa magari hayo
yapelekwe Dodoma kwa sababu lisingekuwa
jambo la busara kwa Serikali kutumia fedha
za umma kununua magari mengine mapya
wakati yale ya Tume bado yanafaa kufanya
kazi na wala hakuna bajeti ya kufanya
manunuzi ya magari mapya.
Hivyo, ni kweli magari hayo yako Ikulu, Dar
es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa taratibu
za kuyapeleka Bunge Maalum la Katiba mjini
Dodoma.
(d) Wajumbe wa Tume kulipwa kiinua
mgongo cha Sh.milioni 200 kila mjumbe
Hakuna shaka kuwa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba wamefanya kazi nzuri
sana na wanastahili pongezi nyingi za
wananchi. Lakini kama wanadhani kuwa
Serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe
kiinua mgongo cha Sh. milioni 200 basi
wanajidanganya. Wala wananchi wa Tanzania
hawawezi kuelewa maana kabisa ya malipo
hayo makubwa kupindukia.
Alichokizungumza Rais Kikwete tokea mwanzo
wa mchakato ni kwamba atafikiria kuwalipa
wajumbe wa Tume aina fulani ya kifuta jasho
ambacho kiwango chake atakiamua yeye na
kwa wakati mwafaka na kulingana na raslimali
za Serikali. Mpaka sasa hajafanya uamuzi juu
ya jambo hili.
(e) Posho ya Sh.500,000 kutwa kwa kila
mjumbe wa Tume
Ikulu pia inapenda kutoa ufafanuzi wa habari
zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya
habari kuwa wajumbe wa Tume hiyo walikuwa
wanalipwa Sh. 500,000 (Laki tano) kama
posho ya vikao kwa siku. Hili nalo siyo la
kweli.
Ukweli ni kwamba wajumbe wa Tume
walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama posho
ya vikao kwa siku. Maofisa waandamizi wa
Tume hiyo walikuwa pia wanalipwa posho ya
Sh. 200,000 (Laki mbili) kwa siku, maofisa wa
kati walikuwa wanalipwa Sh. 150,000 kutwa
na maofisa wa ngazi za chini walikuwa
wanalipwa Sh. 100,000 kwa siku kulingana na
taratibu za Serikali. Anayetangaza vinginevyo
anajaribu tu kuwapotosha wananchi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
02 Aprili, 2014
N B: Vita hii ya Ikulu na maneno yote
haya na majibizano, kwa faida ya nani na
kwa maslahi ya nani? Najiuliza sipati jibu!
Tujadiliane

No comments:

Post a Comment