Wakati Polisi mkoani Iringa imepiga
marufuku helikopta za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, unaotarajiwa kufanyika
kesho, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe amesema yupo
tayari kufa angani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, aliyasema hayo jana
wakati akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa kuhusu hali ya
usalama na polisi walivyojipanga kukabiliana na matukio ya vurugu
yanayotishia uvunjifu wa amani kwenye uchaguzi huo.
Alisema kuwa hakuna chama chochote cha siasa kinachoruhusiwa kurusha
helikopta angani siku ya Jumapili kwa kuwa hatua hiyo ni sehemu ya
kampeni ambazo kisheria NEC imeweka ukomo ambao ni Machi 15, saa 12:00
jioni.
Mungi alisema chama ambacho kitarusha helikopta hizo kwa kisingizio cha
kulinda kura zao ni kuvunja sheria kwa kuwa kura hizo zinalindwa na
mawakala waliotajwa kwenye sheria ya uchaguzi.
MBOWE: NIPO TAYARI KUFIA ANGANI
Mbowe, akizungumza katika mkutano wa kampeni kijiji cha Sadani, alisema
kauli ya kamanda wa polisi Iringa kuzuia chopa yao ni mkakati wa kutaka
kusababisha maafa na yupo tayari kufia angani siku ya Jumapili.
"Tutaruka kwa chopa mbili, RPC Mungi apende asipende niko tayari
kufa...Nazungumza kwa mamlaka kama kiongozi mwenye dhamana. Nchi hii
kila mtu ana haki ya kutumia usafiri wowote...Hatutaogopa kuruka kwa
chopa, mpeni salam kamanda wa polisi," alisema Mbowe.
NEC YATOA UFAFANUZI
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian
Lubuva, akizungumzia matumizi ya chopa yaliyotangazwa na Chadema,
alisema kuwa chombo chochote ambacho kilitumika katika kampeni hizo,
kikiwa na nembo au bango la chama chochote cha kisiasa hakitakiwi kwenye
uchaguzi huo, isipokuwa kama vitaondolewa vitu hivyo, vinaruhusiwa
kutumika.
"Tunachosisitiza hapa ni material (nyenzo) ambazo zilikuwa zikitumiwa
wakati wa kampeni na hatuhitaji kuona nguo, kofia wala magwanda siku
hiyo...Matumizi ya chopa sisi kama tume, hatujakataa kutumika lakini
tunasema kama itatumika kubeba abiria kutoka uwanja fulani kwenda sehemu
nyingine na si kutua kwenye kituo cha kupigia kura, hapo ni
sawa,"alisema Jaji Lubuva.
Alisema ni vigumu NEC kuijibia polisi kuhusu katazo la matumizi ya
helikopta hizo siku ya uchaguzi lakini ukweli ni kwamba kama wataweza
kutofautisha mambo waliyokuwa wakiyafanya katika kampeni zao na uchaguzi
huo, wanaweza kuitumia.
Hata hivyo, Meneja kampeni za Chadema jimbo la Kalenga, Godbless Lema,
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, alisema chopa ya Chadema
inayomilikiwa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, itapasua
anga kama kawaida ikiwa imembeba mgombea wao, Grace Tendega na viongozi
wengine wa chama hicho.
"Tutaitumia helikopta yetu kusambaza chakula na maji kwa mawakala wetu
katika vituo 216 vilivyotengwa. Helikopta ni usafiri kama gari ambalo
wanatumia CCM au Chadema katika kampeni hizi...CCM wana magari yao
ambayo ni Land Cruizer na Chadema tunazo Ford Ranger halafu yameruhusiwa
kutumika lakini chopa hawataki; kwani nani asiyejua lipi ni la
nani,"alihoji Lema.
Alisema Chadema itaheshimu sheria za uchaguzi kwa kuondoa nembo na alama
za kichama katika helikopta hiyo na kuitumia kufanya kazi muhimu
ikiwamo kumsaidia mgombea kuvifikia vituo vilivyopo mbali katika jimbo
hilo.
Alisema hata kama vyombo vya dola vinakazana kuzuia matumizi hayo ya
helikopta, Chadema pia imejipanga kuzuia uhalifu wowote katika jimbo
hilo lakini pia wanategemea kuongeza idadi ya vijana wengine 1,000,
watakaongeza nguvu kwenye kata zote 13.
DAFTARI LA WAPIGA KURA
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Operesheni na Oganaizesheni za Chadema,
Benson Kigaila alisema NEC inajaribu kuficha ukweli kuhusu uboreshaji wa
daftari la wapiga kura kwa sababu imeongeza kinyemela majina ya watu
zaidi ya 1,000 katika daftari la wapiga kura bila ya kutangaza kwa umma
na kuvishirikisha vyama shiriki katika uchaguzi huo.
"Kwa nini daftari hili liboreshwe Kalenga tu, halafu wasitangaze umma
ukajua au kuvishirikisha vyama vinavyoshiriki uchaguzi huu. Huku kuna
maanisha nini kama si hujuma lakini pia hadi jana kuna mawakala zaidi ya
nusu walikuwa hawajaapishwa,"Alisema Kigaila.
Alisema kufuatia ucheleweshaji huo, mawakala wao kama watakuwa
hawajaapishwa hadi Jumamosi, Chadema kinaitaka Tume ya Jaji Lubuva
kuwaapisha wakiwa kwenye vituo vyao kwa sababu hawatakubali kama chama
vituo hivyo vikabaki wazi kwa minajili ya kusubiri mihuri.
RC SENDIGA ATOA ONYO KWA WANAWAKE VIONGOZI: ‘TUKIRUDI NYUMBANI SISI NI WAKE’
-
*Manyara — Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, amewataka
wanawake wakiwemo viongozi kutambua na kuheshimu nafasi zao ndani ya ndoa,
akisi...
50 minutes ago
0 Comments:
Post a Comment