HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE,
WAKATI
WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA, TAREHE 21 MACHI, 2014, DODOMA
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa
Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa
Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa
Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi
Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni
waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya
kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania
wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya
kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama
na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza
Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo
tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu.
Matumaini yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza
vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake
muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa
bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia
ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba
nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu
za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa
changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa
kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja, upendo,
ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya
tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au tofauti
za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba
itakayodumisha amani, usalama na utulivu nchini. Katiba itakayostawisha
zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora
na kudhibiti maovu.
Na,
mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira
mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na
maendeleo yatayopatikana.
Historia
ya Katiba Nchini
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii
itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara
ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti
na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi
zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba
mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya Katiba.
Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya
taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za
Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato
huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum
linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201
wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya
Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia
kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa
kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tangu
kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko
hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi,
kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Kwa
ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
1.
Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia
kufa kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
2.
Mabadiliko ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya
Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri
ya Muungano.
3.
Mabadiliko ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya
Urais ambao haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu
(Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile,
Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya
ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
4.
Mwaka 1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi
vya Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu
wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya
wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya
Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura
ya kutokuwa na imani.
5.
Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais
kupitia Mgombea Mwenza.
6.
Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua
wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu
wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kufanyika
kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko
kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo
na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia
ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha
Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua
mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai
ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti kwamba,
itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato
wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika
kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili
kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi
wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo
tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa
kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa
na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia,
dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka
katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tarehe
16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga
Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja mmoja
na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia Mabaraza ya Katiba.
Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya itakayofikishwa
kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa. Mchakato
wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya maoni ya kuamua
kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe
6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe
2 Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na
kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu
ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa
Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe
18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili, kuamua na kutunga Katiba
mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi
wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Rasimu
ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine
yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu
ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma.
Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu
ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu.
Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni
yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa demokrasia
imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako
huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi
kwa Tume
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na
nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa
nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza
Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki
katikati ya mchakato.
Pamoja
na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote
nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa
maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka
kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi,
kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya
kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele
ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi
wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa
kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi
ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume
imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la
Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa
mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba
ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa, imejumuisha
dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao na
kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za kawaida
za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza mambo
mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe
Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Waheshimiwa
Wajumbe;
Rasimu
ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa
106, sura 17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na
kuelewa vizuri kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi.
Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura
kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno.
Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba
na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kile
ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa
msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya
hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha,
tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha
madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa.
Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika
nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa katika mchakato huu ni kama
chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika
hatua moja kitaonekana katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba
fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza
kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana
ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo
maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua
ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa
vimekuwa na mambo mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive).
Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba
bali yawe kwenye Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako
mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa
mtu hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable).
Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima
yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba
tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Yapo
pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake,
hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo
athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu
inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa
“Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika
likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha
sehemu yake ya bahari”.
Maelezo
hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya
maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi
nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu
hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua
maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima
mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume
la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano
ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu
hii malengo ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa
kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni.
Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo
uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi,
viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako
chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali
ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri
ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji,
Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru
wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa
Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano
majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati
ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali
tatu, inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili
kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za
nchi washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini
kama mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali mbili, mambo haya mazuri
yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi
wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya
Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo
uandishi katika Rasimu. Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua
mengineyo.
Dhana
Mpya
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili
utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba
mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha
kuhusu kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie
kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa
letu changa.
Mambo
ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo
la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya
“Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa
miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu
hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana
na hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande
kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia
na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe
vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo
cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko.
Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa
Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita
mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua
kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge
kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka
1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja
ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli
anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili
aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie
watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema
jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo
au hapana.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa
Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au
la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha
juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea
yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa
sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni
jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika kuungana
na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu
huo hapa kwetu.
Nachelea
kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu
mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa
bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo
jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa
utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna
za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya
Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho
kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye
kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba wenzao mpaka waondoke.
Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani inayoongezwa na kuanzisha
utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo hili jipya lina tija.
Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa
Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo
wa Muungano
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu
watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu
badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu
lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili.
Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa
kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu linapendekeza
kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo
agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi
wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala
hili. Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi
usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu
tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania
inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba,
mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo
jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu
mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya Nyalali
mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume
ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo
hayakukubaliwa.
Waasisi
wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais
wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano
wa Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo
unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha
Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika
na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Natambua
kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu.
Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na
Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana
kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia
kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi
hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei
haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai
yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili
mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali
mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje!
Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make
an informed decision).
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume
imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu
ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar
na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni,
yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali
ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono
muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa
majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa
Serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Sababu
hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii.
Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema
Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa
Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa
ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema
kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa
Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820
au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo
wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa
Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.
Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni
wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Wanasema
pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na
67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu
Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka
muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia
25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza
Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi
wake upi?
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Takwimu
za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211.
Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano
na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo
basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera
Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni
na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia
Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni
yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi,
wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu
uko wapi?”
Changamoto
za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa
kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi
za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo
wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile kinachoitwa
Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo
kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa
hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali
ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa
vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia mkanganyiko kuhusu
ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano baina
ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile,
wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano.
Aidha,
kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka
mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar
kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa
Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika
na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani
ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake,
wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili
Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la
Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge lazima zipelekwe kwenye
Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika Zanzibar. Wananchi
wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi
Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki hiyo Tanzania
Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji wa
mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo baadhi
ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili
muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida
za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya
vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha Washirika
wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na
hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia
unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano
kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo
baina ya washirika na hivyo kusaidia kukuza maendeleo ya nchi.
Faida
za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Pamoja
na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa
muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha
kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali
mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza
gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga uhusiano
na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi wa pande
zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo; na umedumisha
Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake takriban
miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha amani, umoja na
utulivu hapa nchini.
Changamoto
za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Pamoja
na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto
za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto
zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama
kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
alitutoa hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na
mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani kuwa gharama ya
Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (Waulizeni Wazanzibari)
na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila
gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”. Ni matumaini yangu kwamba
katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa
na nyeti.
Tume
imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji
wa gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika.
Vilevile, kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana
juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika
wa Muungano na baina ya nchi washirika na Serikali ya Muungano. Aidha,
upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za kimaendeleo baina
ya pande mbili za Muungano kutokana na kila upande kuwa na sera na mipango
tofauti.
Tume
pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa
(nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha
Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs
in decision making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa.
Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali
pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu
kuna maana ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili
zisiue Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Wanaounga
mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto
zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali
tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza maradufu
kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika muundo wa
sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa
ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa
ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia changamoto za Muungano katika
kipindi cha uhai wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika
kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya
Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka
1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati
ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero
zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa
yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na
Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita
tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika
hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1.
Mgawanyo wa mapato:
(a)
Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b)
Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
2.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3.
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4.
Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5.
Usajili wa vyombo vya moto.
6.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Serikali
zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa mabadiliko
ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
1.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
2.
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
3.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali kadhalika,
katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018
ni nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba
ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini
na kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini
tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha
ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kuhusu
orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda kuwahakikishia
kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazina
kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika.
Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila
za Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo
yake ya ndani. Na, wala siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika
kutetea maslahi ya nchi yao. La hasha.
Pili,
naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya
Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika
na pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa
kwenye Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria
zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi
ulifanywa na Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za
kila upande wa Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la
Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri
mkazisome ili mpate kujua ukweli na undani wa kila kilichoongezwa na
sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nchi
zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo
ni haya yafuatayo:
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano,
Mambo ya Nje,
Ulinzi,
Polisi,
Hali ya Hatari,
Uraia,
Uhamiaji,
Biashara ya nje na mikopo,
Utumishi katika Serikali ya Muungano,
Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mambo ya Nje,
Ulinzi,
Polisi,
Hali ya Hatari,
Uraia,
Uhamiaji,
Biashara ya nje na mikopo,
Utumishi katika Serikali ya Muungano,
Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kati
ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi
kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini
na kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano
zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za
kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo
kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
Jambo
la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha
za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika
kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board)
mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika
kuwa na sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki
na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe
na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa
Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10
Juni, 1965.
Tarehe
11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano:-
(a)
Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b)
Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c)
Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10
ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na
mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo
hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa
Hali ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli,
Barabara, Usafiri wa Majini na kadhalika.
Tarehe
22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali
ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia
kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya Muungano,
suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
Tarehe
22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo
la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki
mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la
Taifa mwaka 1973.
Mwaka
1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha
ya Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza
ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15
katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo
hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo
la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu
kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
Tarehe
17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa”
na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi
vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Bila
ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na mazingira
ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na wala siyo
hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya
na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea
ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila yalipotokea mabadiliko katika
uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa
zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba kwa
sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu
zetu mbili za Muungano yaliingizwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mengineyo yaliachiwa kila upande kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa
maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili
tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji
wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ni
msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya
baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya
hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano wetu.
Ndiyo maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni
za biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na imethibitika kuwa Zanzibar
inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa
rasmi mambo hayo na mengineyo tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha
ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali
ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na
gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu
wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein
msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa
fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha Bungeni
Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu, ingeweza
kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza
kukosa majibu.
Hatimaye
wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga
ya “subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika
mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua
kuitoa rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba,
siku hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni
binafsi. Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar
ni suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo
karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba,
kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe
kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar
na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Jambo
lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana
tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na
mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi za nje
bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali.
Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa
kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia
sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali.
Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti la Serikali
ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache kunufaika isivyostahili,
zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar. Serikali zetu
mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa
kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya
yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa
jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo
na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au taasisi
yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake
kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu
mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar bila ya kulazimika
kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Kwa
maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo, utakaohakikisha
kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu yake. Wanaohusika
na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu wao.
Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba ya kuwabana watekelezaji
kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa
bila ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na
ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali
ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria
na kama hapana budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa
kuyaweka mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Waheshimiwa
Wajumbe;
Katika
mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali
tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto
za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya kuzitatua. Tena
yapo maoni ya watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda
muundo wa Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito unaostahili.
Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile
hoja kwamba Serikali ya Muungano inayopendekezwa haikujengeka kwenye
msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za kusimama. Inategemea mno ihsani
ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza kuanguka wakati wowote, na
Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani ya nchi washirika. Tena
inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa washirika amefanya hivyo.
Pili,
kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya
kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa
unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba,
hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano
haina chombo chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo
vya nchi washirika kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli
za Serikali ya Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa
kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo
ya kutoka kwao.
Bahati
mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa
mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana
nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika
mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa
kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana
kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama
chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa
sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali
hiyo kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu
iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa.
Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi
ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano,
Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la kufanya. Kwa kweli
uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu
hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali
tatu unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali
tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na
inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa
hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi
yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza
kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia
inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi washirika. Bila ya shaka Bunge
hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza kuonyesha njia ya kuondoa hofu
hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona kuwa huu ni uthibitisho
wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto
za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Katika
kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko
ya Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa
Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo
(deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo
muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic
sentiments) wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini
sana mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo
tu ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao.
Naona hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto
hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza
kusaidia.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ni
lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami
kwani yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama.
Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana
kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua
kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani
Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano.
Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama
watu wamoja na raia wa nchi moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja
kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya Watanganyika na Wazanzibari na
siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa iliyopita takriban asilimia
90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua
ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza
kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa
utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao
siyo kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata
waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu
mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika
kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa
magumu kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka
huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Changamoto
hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni
za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili
ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012
na watu wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke
Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea
pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu,
baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu
mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui
wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na Muungano
wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Sisi
viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna
budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio
sahihi. Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana,
wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano kusambaratika
halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa
kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi
waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao.
Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu tulichokijenga
kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi
katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993
alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna
hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo
hazisubiri.”
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Siku
moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo
ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila
mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri
msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka
kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine
na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi
Yenu Kubwa
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Mambo
ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza
kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na kwenye
majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu
ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga
Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na itaendeshwa
vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi yetu hatima
njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya kujadili na kuyafanyia
uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya
Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda wa kutafakari kila neno, kila
sentensi, na kila dhana ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya
hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika
sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu.
Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache,
mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya
kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa.
Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba.
Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote.
Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa
nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi
kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi
nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza
la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake
haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza
kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu sote. Anastahili
pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa kanuni.
Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa
Samuel Sitta.
Napenda
pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali
hivyo hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu
hii inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio
yao kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati
wote wa kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo vyenu. Wakati wa
semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya wananchi
wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona
matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno waliyoyasikia kutoka
kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni
matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena
katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na
Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na
wa nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don’t shout)
au kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika kujieleza.
Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile au hata kugombana.
Ni utovu wa uungwana usiotegemewa kutoka kwenu. Tusiwaangushe wananchi
wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni
Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Ombi
langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali
maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi yenu
binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania Kwanza”.
Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo kwa kila
jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi
yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama misimamo
hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata
hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha
mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi
wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza
mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni
kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni watu
usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza kuwepo kitu chenye
manufaa.
Mheshimiwa
Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba
muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya hivyo hamtalazimika
kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi maarifa wale
mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya kushirikiana
na kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute kushindana, hili ni jambo
ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania
wote washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi
wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa kutambua na kuthamini umuhimu
wa kuwa na taratibu za mawasiliano, mashauriano na ushirikiano. Daima
muwe watu wa kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya awali.
Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni
madaraja imara zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa
Mwenyekiti;
Naomba
nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa
dini tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba
uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi
ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila watakaloliamua.
Baada
ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti
kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni
kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza Wajibu
Wako.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment