JESHI la polisi mkoani Arusha limeingia lawamani likituhumiwa kumuua
kwa kumpiga risasi daktari wa kitengo cha ukimwi katika hospitali ya
Selian,Japhet Mtingala alimaarufu Banda(48) mkazi wa Ekenywa wilayani
Arumeru kwa kumhusisha na tukio la ujambazi,ambapo watu wengine watatu
waliouawa wakidaiwa kupanga njama ya kupora fedha katika kituo cha
mafuta.
Aidha inadaiwa kuwa,daktari huyo aliuawa wakati akipeleka dawa ya
kurefusha maisha ARV's kwa mgonjwa aliyekuwa katika bar ya Pama
iliyopo katikati ya jiji baada ya kukubaliana wakutane hapo.
Tukio la kuuawa kwa watu hao lilitokea Februali ,21 mwaka huu,majira
ya saa 1.30 usiku katika bar ya Pama iliyopo katikati ya jiji na
kuthibitishwa na kamanda wa polisi mkoani Arusha ,Liberatus Sabas
akidai ni majambazi waliokuwa wakipanga kwenda kupora.
Sabasi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa majambazi hao walikuwa
watano huku mmoja akifanikiwa kutoroka akiwa na silaha aina ya SMG na
kufanikiwa kupata silaha moja aina ya bastola ikiwa na risasi kadhaa .
Kamanda alionyesha mfuko mmoja aliodai ulikuwa umesheheni risasi.Hata
hivyo taarifa zilizoelezwa na baadhi ya wafanyakazi wenzake katika
kitengo hicho cha ukimwi ,waliutambua mfuko huo kwamba ndio uliokuwa
ukitumiwa na marehemu kubebea dawa za ARV's alizokuwa akiwapelekea
wagonjwa wasio na uwezo wa kufika hospitalini.
Kwa mujibu wa kaka wa marehemu,Joel Samweli,alisema familia imejipanga
kushughulikia suala hilo,kupitia vyombo mbalimbali vya kisheria ili
haki ipatikane ,kwani alisisitiza mdogo wake hakuwa na chembe ya
ujambazi wa aina yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mazishi ya marehemu
Banda,Samwel alilitupia lawama jeshi la polisi mkoani hapa,kwa
kutokuwa makini kutambua walengwa wa uhalifu, badala yake askari wake
waliamua kuwafyatulia risasi bila kuwa na maelekezo sahihi ya
wahusika.
''baada ya mazishi familia itakaa na kukubaliana chakufanya,kwani huu
ni uonevu na utumiaji mbaya wa silaha,pale hapakuwa na majibizano ya
risasi wala kujeruhiwa kwa askari kama alivyosema kamanda wa
polisi,askari wale walikuwa na uwezekano wa kuwakamata na kubaini
wahalifu na sio kuwamiminia risasi''alisema Samweli
Akitoa salamu kwa niaba ya hospitali ya Selian,dkt David Mlaki
alieleza kusikitishwa na tukio hilo la kuuawa kwa muuguzi huyo na
kubainisha pasipo shaka kuwa marehemu hakuwa akijihusisha na matukio
ya ujambazi na kwamba wamepoteza maisha akitoa huduma ya dawa kwa
mgonjwa.
''Kwa kweli tukio hili limetusikitisha sana ,hatuna la kusema
tunamwachia mungu, ndio muweza wa yote,hatuna budi kushukuru kwa kila
jambo,ila marehemu Banda ametuachia pengo kubwa kwani alikuwa mtu
muhimu katika huduma ya ukimwi kwa muda mrefu''alisema Mlaki.
Taarifa zaidi zimethibitika kuwa marehemu Banda,aliondoka
kazini(Selian) majira ya saa 11.30 jioni akiagana na mtumishi
mwenzake(jina linahifadhiwa) kuwa anapeleka dawa kwa wagonjwa aliokuwa
amewasiliano nao kwenye simu.
Habari zinadai kuwa kabla ya kufika eneo la tukio Banda alipitia
sehemu nyingine kutoa dawa kwa mgonjwa mwingine na ulipofika muda huo
ndipo alipoenda katika eneo la tukio na kukutana na mgonjwa wake
ambaye alikuwa mwanamke .
Taarifa zinasema kuwa mwanamke huyo alimkaribisha marehemu katika meza
moja wapo aliokuwa amekaa yeye na watu kadhaa huku mwanamke huyo
akionekana kuwafahamu zaidi watu hao na kumtambulisha kwao.
Baada ya utambuzi huo dakika chache askari polisi walivamia na
kuzingira meza hiyo na kuwataka wajisalimishe,ambapo ilidaiwa kuwa
mmoja wa watu hao alichomoa bastola kwa lengo la kuwafyatulia askari
hao ,ndipo askari hapo walianza kuwamiminia risasi maeneo mbalimbali
huku marehemu Banda akipigwa risasi kadhaa na kufumua kichwani na
mdomo.
Mwili wa daktari huyo umezikwa na mamia ya wakazi wa maeneo mbalimbali
katika shamba lake kijijini kwake na ameacha mke,aitwaye Agnes
Japhet,na watoto wanne ,ambao ni Felister ,Scolla,Justine na
Miriamu,huku mmoja wa watoto wake akisomeshwa kwa ufadhili wa
mwandishi wa habari wa kampuni ya The Guardian, mkaoni Arusha,Cyinthia
Mwilolezi.
▼
No comments:
Post a Comment