MADABIDA APANDISHWA KIZIMBANI KWA ARVs FEKI


image


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano, jana wa mefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka matano.
 

Mashtaka hayo ni kusambaza dawa feki za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV’s) na kuisababishia Bohari Kuu ya Madawa nchini (MSD), hasara ya zaidi ya sh. milioni 148.
 

Washtakiwa wengine ni Seif Salum Shamte, Saimon Alfred Msofe, Fatma Ally Shango, Sadiki Frank Materu na Evance Mwemezi.
 

Hati ya mashtaka ilisomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwasyeba ambapo katika shtaka la kwanza ni kusambaza dawa feki za ARV’s ambalo linawahusisha Madabida kama Mkurugenzi wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd.
 

Washtakiwa wengine ambao shtaka hilo linawahusu ni Msofe ambaye ni Meneja Masoko, Shamte (Mkurugenzi wa Operesheni), na Shango (Mhasibu Msaidizi katika kiwanda hicho).
 

Kimaro alidai, Aprili 5, 2011 washtakiwa hao walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral ambazo ni gramu 200 za Verirapine, Batch namba OC01.85 na Stavudine, gramu 30.
Dawa hizo zilionesha kutengenezwa Machi 2011 na muda wake wa matumizi ulikuwa uishe Februari 2013 wakati wakijua dawa aina ya Antiretroviral, hazikuwa halisi.
Katika shtaka la pili, linawahusu washtaki wa Madabida, Shamte, Msofe na Shango ambao wanadaiwa Novemba 2011, mshtakiwa wa kwanza (Madabida) na Msofe, walisambaza kopo 4,476 za dawa aina ya Stevodium 30mg+Nerviraphin 2oogm+Lamivudine 150gm, zenye namba 0C0185.
Dawa hizo zilionesha kuisha muda wake Februari 2013 wakati si dawa halisi.
Shtaka la tatu pia linawahusu washtakiwa hao wakidaiwa kati ya Aprili 1 2-29,2011 ,jijini Dar es Salaam, walijipatia fedha zaidi ya sh. milioni 148 kwa njia ya udanganyifu kutoka MSD kwa ajili ya malipo ya dawa halisi aina ya Antiretroviral, namba 0c.01 .85, wakati wakitambua si kweli.
Katika shtaka la nne, linawahusu waajiriwa wa MSD ambao ni Materuna Mwemezi ambapo wanadaiwa kati ya Aprili 5, 2011 na Aprili 13, 2011, walifanya uzembe na kushindwa kuzuia dawa hizo zisisambazwe.
Alidai washtakiwa hao ambao mmoja alikuwa kama Ofisa Udhibiti Ubora na Meneja Udhibiti Ubora na kujua nia ya kutendeka kosa la kusambaza dawa hizo, hawakutumia nyadhifa zao kudhibiti kosa hilo.
Shtaka la mwisho linawahusu washitakiwa wote ambapo ilidaiwa Aprili 5, 2011 na Aprili 30,2011, jijini Dar es Salaam, wakiwa na nia mbaya, waliisababishia MSD hasara ya zaidi ya sh. milioni 148 kwa kuidhinisha malipo ya dawa feki namba 0C.01.85.
 

Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mwasyeba, alitoa masharti ya dhamana ambayo ni kila mashtakiwa kuweka fedha taslimu mahakamani, mali isiyo hamishika yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 12 na wadhamini wawili. 

Mshtakiwa Madabida na Materu, waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimia masharti wengine walipelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti. Kesi itatajwa tena Februari 24, mwaka huu.

0 Comments:

Post a Comment