MBUNGE wa Msalala, Ezekiel Maige, (CCM) amesema kuwa mifumo mibovu ya uendeshaji iliyopo
Serikalini inasababisha baadhi ya wizara kukumbwa na misukosuko ambapo imefikia
hatua Wizara ya Maliasili na Utalii inafahamika
kama ya “kuchinja” mawaziri na na ile ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuwa
ya kutia Mawaziri “kashikashi”.
Aliyasema hayo jana jijini hapa mara baada ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, (LAAC) kupokea taarifa ya
halmashauri ya jiji la Arusha.
Maige
ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kabla ya kujiuzulu
huku akilalamika kuonewa alisema kuwa mifumo iliyopo kwa sasa
haiwawezeshi
Mawaziri au Makatibu Wakuu kujua utendaji wa wafanyakazi walio chini yao
ili
kuwawezesha kuwapandisha vyeo kutokana na utendaji badala yake hufanya
maamuzi kwa
kuzingatia majungu wanayopelekewa.
Alisema kuwa ni vema suala la nidhamu ya wafanyakazi likazingatiwa
katika jitihada za kukabiliana na tatizo la ubadhirifu wa fedha za umma ambapo
alishauri ni vema ofisi ya mkuu wa mkoa ikatumika kama ngazi ya nidhamu kwa
watendaji wa halmashauri zilizopo kwenye mkoa husika badala ya mamlaka hayo
kuwa wizarani.
“Haiwezekani mtu akafuja fedha kwenye halmashauri halafu
akatakiwa kubeba nyaraka zake akajieleze kwenye mamlaka yake ya nidhamu iliyopo
Dodoma, ndiyo tunaona wanaenda kule badala ya kuwajibishwa wanatoa rushwa
wanahamishiwa halmashauri nyingine” alisema Maige.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa TAMISEMI, Kasim Majaliwa aliwataka
wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanawaelimisha watumishi wao waliokaribia
kustaafu kuhakikisha wanarudisha fedha za mishahara zitakazowekwa kimakosa
kwenye akaunti zao pindi wanapostaafu.
“Waelimisheni wastaafu wakiona wamestaafu lakini mshahara
unaendelea kuingia kwenye akaunti zao ni vema wakazirudisha vinginevyo watakuja
kukatwa fedha hizo kwenye malipo ya mafao yao ya mwisho” alisema naibu Waziri
huyo.
Alipongeza uamuzi wa Halmashauri ya jiji la Arusha kwa mkakati
waliyojiwekea wa kuhakikisha nyumba za udongo zinaondoka katikati ya jiji
ambapo alishauri halmashauri nyingine kuiga mfano huo na kwenda mbali zaidi kwa
kuangalia uwezekano wa kuwakopesha ili waweze kujenga nyumba bora za kuishi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajab Mbaruku alisema
kuwa wajumbe wa kamati hiyo wamejikita katika kutafuta matatizo yaliyopo kwenye
halmashauri hiyo ili waweze kuishauri serikali namna ya kuboresha na si kupiga
kelele.
No comments:
Post a Comment