MMOJA kati ya madiwani watano walifukuzwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyekuwa anawakilisha kata ya Elerai, jiji ni Arusha, John Bayo ametangaza kujiunga na Chama Cha Wananchi (CUF).
Alitangaza kujiunga kwenye chama hicho Septemba 30,mwaka huu kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyikia kwenye viwanja vya Kilombero ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama hicho akiwemo Mwenyekiti wake, Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Bayo alisema kuwa yeye aliwahi kuwa mwanachama wa CUF mwaka 1992 na alishiriki kutafuta wadhamini wa chama hicho kukiwezesha kupata usajili wa kudumu hivyo ameamua kurudi nyumbani baada ya kuchoshwa na siasa za fujo.
Alisema kuwa alisIkitishwa na uamuzi wa Kamati kuu ya Chadema yenye wajumbe 45 wa kumfukuza uanachama bila kuwauliza wananchi wake waliomchagua huku akiendelea kulalamika kuwa hata waasisi wa Chadema walijaribu kutafuta suluhu kwa kuwashauri madiwani hao kufuta kesi waliyokifungulia chama hicho mahakamani ili wamalize suala hilo wakatekeleza lakini Chadema imeshindwa kuwarudishia uanachama kutokana na mtu mmoja aliyedai kuwa mbishi anayesikilizwa na viongozi kuendelea na msimamo wa kuwagomea.
Kwa upande wake katibu wa Chadema mkoani hapa akiongea na Tanzania Daima kwa njia ya simu alisema kuwa anamtakia safari njema diwani huyo wa zamani kwani Chadema kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa mujibu wa katiba yake na hivyo wanachama na viongozi wa ngazi yoyote wanapaswa kuzifuata na kuziheshimu na anayeona anashindwa ni vema akachukua uamuzi wa kuondoka kama Bayo.
Alisema kuwa hata waasisi wa Chadema waliwataka madiwani hao wazingatie taratibu na kanuni za chama ikiwemo kuomba radhi lakini walishindwa kufuata taratibu za chama na hawakuheshimu maamuzi ya vikao vya juu ikiwemo kile cha kamati kuu huku akisistiza kuwa Chadema kinataka kujenga chama chenye adabu, wanachama, viongozi na wawakilishi wenye adabu anayeona hawezi ni bora akaondoka.
CUF WABEBA WANANCHI KWA MABASI TOKA JIJINI DAR
KATIKA hatua nyingine mkutano huo ulijaa wananchi walioletwa na mabasi kutoka wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke za jijini Dar Es salaam pamoja na viongozi Tanga Mjini, Arumeru, Singida, Handeni na moshi.
Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Siasa wa CUF aliyasema hayo wakati akitoa utambulisho juu ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ambapo alisema mkuwa ameelezwa kuwa wilaya hizo mbali ya kuleta viongozi pia wameleta idadi kubwa ya wanachama.
Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya magari ya abiria aina ya Coaster yaliyowaleta wanachama hao yakiwa yameegeshwa pembeni ya uwanja wa mkutano yenye namba za usajili T 941 CAK, T 992 BEK, T 393 AXY na T 477 BXA huku yakiwa na wamefungwa bendera za CUF mbele na nyuma ambapo mawili aina ya mafuso marefu namba zake hazikuweza kuonekana kutokana na kuzibwa na bendera hizo ambapo mara baada ya mkutano kumalizika abiria wa magari hayo walitangaziwa kuwa warudi kwenye magari yao tayari kwa ajili ya kuanza safari leo (jumatatu) asubuhi.
Katika hatua nyingine Maalim Seif ambaye ni makamu wa Rais wa Zanzibar alifika mkutanoni hapo majira ya saa 3:46 alasiri akiwa na msafara wa magari ya serikali ikiwemo lile alilopanda yeye lenye nembo ya ikulu pamoja na yale yaliyomsindikiza ambayo yanaonekanaga kwenye misafara ya viongozi wa kitaifa likiwemo lile lenye namba za usajili T 504 BSJ ambalo lilikuwa na maafisa usalama wa Taifa.
No comments:
Post a Comment