MWANASHERIA wa halmashauri ya jiji la Arusha, Allen Ndomba anadaiwa kufanya uamuzi binafsi wa kuwataka madereva wa bodaboda jiji hapa kulipa ushuru wa maegesho wa shilingi 500 hali iliyoibua taharuki kutoka kwa madereva hao wakipinga agizo hilo hivyo kusitisha kutoa huduma kwa saa kadhaa.
Tangazo hilo ambalo kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Estomih Chang’a alitangaza kulibatilisha pia liliibua maswali mengi kutoka kwa baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo kwa kile walichoeleza kuwa hakuna kikao cha baraza la madiwani kilichokaa kujadili na kupitisha ushuru huo hivyo kuhoji watumishi wa halmashauri hiyo walipata wapi mamlaka ya kuamua.
Chang’a aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa awali alipopata taarifa juu ya tangazo hilo alifikiri limetolewa na kampuni ya uwakala wa maegesho ya halmashauri hiyo lakini alishangaa kukuta limeandikwa kwa pamoja na mwanasheria wa halmashauri hiyo ambapo alidai kwa sasa mtumishi huyo anashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi umma.
“Mwanasheria wangu alichukua uamuzi ambao haukumuhusu wala hakunishirikisha, sisi kwa kushirikiana na jeshi la polisi na Sumatra tuko kwenye mchakato wa kujadili namna ya kuboresha mazingira ya wandesha biashara ya bodaboda kwa kuangalia ni maeneo gani yatumike kwa ajili ya maegesho yao, hili la ushuru mwanasheria wangu tunaendelea na taratibu za kumchukulia hatua kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma” alisisitiza Chang’a.
Alisema kuwa madereva wa bodaboda ni wadau wa halmashauri hiyo kwani wanaelewa kuwa ni wafanyabiashara wa kipato kidogo hivyo hawawezi kuwajengea mazingira magumu ya kuendesha shughuli hiyo ambayo yanaweza kuwasababisha washindwe kwa kile alichodai kuwa inaweza kuwasababisha wengine kuachana na biashara hiyo inayowaingizia kipato chao halali na kuwafanya kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu.
Awali madereva wa bodaboda walikutana eneo la Sakina chini ya mwenyekiti wao, Godlight Reubenalile ambaye alisema kuwa hawako tayari kulipa ushuru huo wa shilingi 500 kwa siku kwani ni mkubwa mno ambapo kwa mwaka watakuwa wamelipa zaidi ya shilingi 180,000.
Walisema kuwa serikali iliamua kuwaondolea kodi waliyokuwa wakitozwa na mamlaka ya mapato nchini (TRA) ya shilingi 35,000 kwa mwaka baada ya kuona ilikuwa ni kodi ya manyanyaso kwao kwani kiwango kilikuwa kikubwa jambo alilohoji iweje halmashauri inaamua kuwatoza mara tano zaidi ya kile kilichoonekana kuwa ni kigumu kwao kulipa.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Levelosi, Ephata Nanyaro akiongea na Tanzania Daima kuhusiana na suala hilo aliwataka madereva hao kutolipa ushuru huo kwa kile alichodai kuwa hawakuwahi kujadili suala hilo kwenye vikao vya baraza la madiwani hivyo tangazo la kupandisha ushuru siyo halali hata kidogo.
“Halmashauri hukusanya kati ya asilimia 20 hadi 38 ya makisio ya makunyo tunayojiwekea, hata hayo yanayokusanywa hayafikishwi kunakotakiwa na hili linathibitishwa na hati chafu tuliyopatiwa, nadhani badala ya kufikiria kuanza kuwabebesha mzigo watu wa bodaboda , watendaji wangeongeza nguvu na uadilifu ili ili waongeze makusanyo walau yafikie asilimia 98 kutokana kwa vyanzo vilivyopo” alisema Nanyaro.
No comments:
Post a Comment