IMEELEZWA kuwa kuongezeka kwa bei ya meno ya tembo na pembe za kwenye nchi za bara la Asia kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matukio ya ujangili hapa nchini.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi mkuu wa hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), Allan Kijazi wakati akifungua semina ya waandishi wa habari kanda ya kaskazini juu ya uhamasishaji wa utalii wa ndani kwenye hoteli ya kitalii ya Sal Sanero , Moshi.
Alisema kuwa meno ya tembo hununuliwa kwa wastani wa dola 1,000 kwa kilogram moja ( sawa na zaidi ya sh. 1,500,000) kwenye nchi za China, Japan, Taiwan na India ambazo uchumi wake umekuwa sana jambo alilosema kuwa limechangia kuongeza mtandao wa ujangili .
Kijazi alisema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo katika kudhibiti ujangili huo ambao hufanyika kwa mtandao wa kimataifa unaowashirikisha majangili toka ndani na nje ya nchi huku wafadhili wao wakiwa kwenye nchi hizo za bara la Asia.
Hata hivyo alisema kuwa TANAPA wamejizatiti kukabiliana na ujangili huo huku akisistiza umuhimu wa wananchi wote kushiriki kikamilifu kulinda rasilimali za Taifa kwa kutoa tarifa za majangili pindi wanapowabaini kwenye maeneo yao.
“Kwa sasa tunashirikiana na polisi wa kimataifa(Interpol) kufuatilia mtandao huu huko nje ya nchi ili tuweze kuwapata watuhumiwa sugu pamoja na vithibitisho vitakavyotuwezesha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria” alisema mkurugenzi mkuu huyo wa Tanapa wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Alisema kuwa wameamua kushirikiana na vyombo vya kiintelijensia vya kimataifa ili kuwawezesha kuwapata wale wanaofadhili mitandao hiyo ya kijangili kwani tofauti na hivyo wataishia kukamata wapagazi waliotumwa kubeba nyara hizo jambo ambalo haliwezi kumaliza tatizo hilo.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea hifadhi za Taifa ili kujionea vivutio vivyopo kwa kile alichosema kuwa kwa sasa wananchi wachache sana sawa na asilimia 2 tu ya watu wanaotembelea hifadhi hapa nchini huku asilimia 98 ikiwa ni watu kutoka nje ya nchi.
Kijazi alisema kuwa kwa sasa asilimia 70 ya watalii wanakuja nchini hutembelea hifadhi za kaskazini za Kilimanjaro, Tarangire, Manyara, Serengeti na Arusha huku wakishindwa kufika kwenye hifadhi za magharibi na kusini mwa nchi kutokana na miundo mbinu ya barabara kutokuwa nzuri.
0 Comments:
Post a Comment