WATOTO wenye ulemavu wameiomba Serikali kuweka alama maalum kwenye barabara kwa kuzingatia makundi yote ya walemavu ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali kupita kwa urahisi tofauti na sasa ambapo alama hizo zimezingatia walemavu wa viungo pekee.
Waliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwenye viwanja vya Sheh Amri Abeid wakati mwanafunzi wa Shule ya Msingi Meru Kitengo cha Viziwi alipokuwa akisoma risala.
Alisema kuwa watoto wenye ulemevu wa kuona hupata shida wakati wa kuvuka barabara kutokana na alama nyingi zilizoko sasa kutoa kipaumbe kwa walemavu wa viungo.
Watoto hao waliomba Serikali kuhakikisha inawapangia waalimu wanaohitimu mafunzo kwa ajili ya shule maalum kwenye shule husika ili kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu kwa uhakika hasa wale wenye matatizo ya kuona ambao husoma kwa kutumia maandishi maalum.
Aidha waliwaomba walezi kutowatelekeza watoto wenye ulemavu bali wawaape huduma na malezi bora kama wale wengine kwa kuhakikishia wanawapatia mahitaji muhimu ikiemo elimu, chakula huku wakisisitizia kuvalishwa nguo zinazozingatia maadili.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la Kiserikali la linashughulikia masuala ya haki za kisheria, maendeleo ua jamii na uchumi kwa watu wenye ulemavu, (DOLASED), Gidion Mandes aliwataka wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuhakikisha wanawatoa watoto hao kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa inayotazamiwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu.
Alisema kuwa itaiwezesha Serikali kujua idadi ya walemavu waliopo nchini hivyo kurahisisha uandaaji wa mipango ya maendeleo kwa ajili yao.
Kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu “Haki za Watoto Wenye Ulemavu ni Jukumu letu kuzilinda na kuziheshimu” watoto kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Arusha walijumuika kwenye maandamano yaliyoanzia kwenye ofisi za mkuu wa mkoa mpaka kwenye viwanja hivyo yakiongozwa na bendi ya shule ya msingi ya Uhuru.
0 Comments:
Post a Comment