Friday, June 29, 2012

WAFUGAJI WAWINDAJI WA ASILI WATOA VIPAUMBELE VYAO KWENYE KATIBA MPYA



JAMII za wafugaji na wawindaji asili wameeleza vipaumbele saba juu ya mambo wanayopendelea yaingie kwenye katiba mpya yakijikita katika masuala ya ardhi, fidia na  ulinzi kwa jamii za wawindaji wa asili ambao wako hatarini kutoweka.

Aidha wanapendekeza katiba mpya iweke usimamizi wa ardhi mikononi mwa taasisi za kiwakilishi au za kidemokrasia tofauti na sasa ambapo usimamizi wa raslimali uko chini ya Rais na vyombo vya serikali kuu.


Mratibu wa katiba initiative, (KAI),  William Olenasha aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa chombo hicho kilichoundwa ikiwa ni utekelezaji wa  maazimio ya mkutano mkubwa  wa viongozi mbalimbali wa jamii za kifugaji na wawindaji wa asili ulioitishwa na asasi  za PINGOs Forum na ALAPA Novemba 2011.

Alisema kuwa kutokana na  mchakato wa katiba kuwa ni fursa adhimu ya kutafutia ufumbuzi wa matatizo yanayokabili jamii za kifugaji na wawindaji wa asili ndiyo maana wakaunda KAI yenye jukumu la kutoa elimu na kuwahamasisha watu wa jamii hizo kujitokeza kushiriki mchakato wa katiba mpya ikiwemo kutoa maoni kwenye tume ya katiba.


Alitaja vipaumbele hivyo vilivyotokana na maoni yaliyotolewa kwenye mikutano mbalimbali iliyoandaliwa na KAI pamoja na NGO’s zaidi ya 30  ambapo wanataka katiba mpya iweke utaratibu maalum wa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ufugaji kama ambavyo kwa sasa yametengwa maeneo maalum kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na misitu sanjari na kutambua ufugaji kama shughuli ya kiuchumi.

“Kuna wakati fulani mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere alisema kwamba tumetenga maeneo kwa ajili ya nyumbu lakini hatujatenga maeneo yoyote  kwa ajili ya wafugaji wetu. Katiba mpya ni fursa ya kurekebisha makosa haya  kwa kutenga maeneo maalum kwa  ya ufugaji” alisistiza Olenasha.
  


KAI ilieleza kuwa ni vema ardhi na rasilimali za Taifa zikapewa ulinzi kikatiba kwa kuweka vipengele vinavyozuia ugawaji au utoaji wa ardhi holela bila kuwashirikisha wananchi jambo alilosema kuwa litasaidia kuondokana na tatizo la wafugaji kuondolewa kwenye maeneo yao kama ilivyo sasa.

Pia jamii hizo za wafugaji na wawindaji walipendekeza katiba mpya itambue ardhi ya jamii(community lands) tofauti na utaratibu wa sasa unaotambua ardhi za vijiji hivyo haulindi haki za ardhi za jamii zenye watu wachache   kama Wahadzabe na Ndorobo ambao kwa sababu ya idadi yao kuwa ndogo hawawezi kulinda  haki na maslahi yao  katika ardhi pale wanapokuwa na makundi mengine kwenye  vijiji.

“Hali  ya wawindaji wa asili ni ya kusikitisha sana na wengi wamo hatarani kupotea katika uso wa dunia kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kuwanusuru.  Baadhi ya makabila yamepungua sana kiasi kwamba kuna wengine ambao idadi yake haifiki hata  2,000. Ni vizuri katiba mpya ikatambua kuwa kuna Watanzania ambao wanahitaji nguvu za ziada ili kuweza kuwanusuru wasije kutoweka  kwenye uso wa dunia”

“Kama tumeweza kulinda aina ya wanyama walio hatarini kupotea(endangered animal species) kama faru si vibaya vile vile kutambua  kuwa  kuna Watanzania ambao ni ‘endangered communities’. Tutegemea kwamba katiba mpya itatambua makundi haya pamoja na kuweka namna za kuwapatia ulinzi” alisisitiza Olenasha.


Naye mgeni rasmi kwenye hafla hiyo mwenyekiti wa Jukaa la Katiba, Deus Kibamba, aliitaka KAI kuhakikisha inawahamasisha wadau wao kushiriki kwenye mchakato wa katiba kikamifu ikiwemo kujitokeza waweze kupendekezwa kuunda bunge maalum la katiba ili kuweza kuhakikisha inapatikana katiba inayokidhi matakwa yao.

Kwa upande wake mkurugenzi wa PINGO’s Edward Porokwa alisema kuwa jamii za wafungaji na wawindaji wa asili wameachwa nyuma kimaendeleo hivyo wanamahitaji tofauti na yale ya kiujumla ndiyo maana wameamua kuanisha maeneo maalum kwa ajili yao kabla ya kuingia kuzungumzia maeneo mengine yanayoshirikisha Watanzania kwa ujumla kama masuala utawala bora, madaraka ya Rais pamoja na uhuru wa mahakama.


No comments:

Post a Comment