Wednesday, June 20, 2012

MAISHA YANGU YAKO HATARINI- MWALE


WAKILI maarufu nchini, Median Mwalle, amesema kuwa maisha yake yako hatarini kutokana na kitendo cha watu mbalimbali wakishirikiana na mawakili wa serikali kumfuata kwenye mahabusu ya Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha la Kisongo wakitaka wamchuke kumpeleka kusikojulikana.

Mwale ambaye yupo rumande  kwenye gereza hilo kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana, alitoa malalamiko hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Msofe, wakati akiahirisha kesi hiyo ya jinai namba 330/11 kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Charles Magesa, anayesikiliza shauri hilo ambapo upande wa serikali uliwakilishwa na mawakili Fredrick Manyanda na Neema Ringo.

Mwalle ambaye aliomba kuongea baada ya wakili wake, Loom Ojare, kuwa kwenye shauri jingine, alisema kuwa amelazimika kutoa taarifa hiyo kwani jambo lolote baya linaweza kumpata wakati wowote kutokana na matukio ya kufuatwa gerezani kwa sababu ambazo haziko wazi.

“Maisha yangu yako hatarini, nafuatwa magereza na watu wakiwamo hawa mawakili (huku akiwaonyesha mawakili wa serikali), pamoja na kwamba hakimu anayesikiliza shauri hili hayupo, naomba iwekwe kwenye kumbukumbu za mahakama, kwa sababu sijui ni wapi wanataka kunipeleka na nini kitanitokea leo au kesho,” alidai Wakili Mwalle.

Licha ya Hakimu Msofe kukubaliana na hoja ya umuhimu wa mshitakiwa huyo kuieleza mahakama mambo anayohisi ni hatari kwa maisha yake, lakini alishauri yawasilishwe mbele ya hakimu anayesikiliza shauri hilo ili aweze kufanya maamuzi na hivyo kuamua kupanga shauri hilo kutajwa Machi 28 mwaka huu kutoa fursa kwa Mwale kuwasilisha malalamiko yake.

Malalamiko ya wakili huyo yamekuja siku chache baaada ya mahakama hiyo kuwaagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DPP), Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha kuyarudisha magari saba na simu za mkononi kwa wakili huyo maarufu mkoani Arusha, Mediam Mwale, anayetuhumiwa kupatikana na fedha chafu.

Uamuzi huo ulitolewa na  Hakimu Mkazi Mfawidhi  Magesa, ambaye alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, mahakama yake imeridhika kuwa mamlaka hizo zilikamata magari hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act) pamoja na vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya mwenendo wa kesi za jinai.

“Ukamataji  huo ni kinyume cha sheria kutokana na kitendo cha upande wa mashitaka kukamata magari hayo bila kufuata taratibu zinazokubalika kisheria.

“Mahakama inaamuru Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai  nchini, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa TRA nchini na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha ambao walihusika katika zoezi la ukamataji kuhakikisha wanayarudisha magari yote kwa mshitakiwa nyumbani kwake walikoyachukua,” aliamuru Hakimu Magesa.

Magari yaliyoamriwa na mahakama kurejeshwa kwa Mwale ni T 690 BEW aina ya Range Rover, T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS Cadillac Escalade, T 499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo yalichukuliwa Novemba mosi, pamoja na gari  T 660 BCG Toyota Chaser lililokamatwa Desemba 8, mwaka jana.

Hata hivyo, hadi jana utekelezaji wa uamuzi huo wa kuyaachia magari ya wakili Mwalle ulikuwa haujafanywa na mamlaka zilizoagizwa kufanya hivyo.


No comments:

Post a Comment