Saturday, June 30, 2012

HAKIMU KESI YA MWALE AWAONYA MAWAKILI WA SERIKALI

HAKIMU mkazi mfawidhi, Charles Magesa jana aliwacharukia mawakili wakuu wa Serikali , Fredrick Manyanda na Neema Ringo akiwataka kuacha kutumia vibaya fedha za walipa kodi kwa kuamua kuchelewesha kwa makusudi kuendelea kusikilizwa kwa kesi inayomkabili wakili maarufu nchini, Median Mwale kwa kisingizio cha kusubiri nyaraka kutoka Marekani.

Aidha  ametupilia mbali maombi ya mawakili hao wa Serikali waliomtaka kujitoa kwenye shauri hilo kwa kile alichoeleza kuwa hoja walizozitoa hazikuzingatia sheria wala hazikuwa na ushahidi huku akiiagiza mamlaka ya mapato nchini (TRA) kutekeleza amri halali ya mahakama hiyo ya kumpatia Mwale magari yake saba kwani mpaka sasa hakuna mahakama ya juu iliyofuta amri hiyo.

Hakimu Magesa aliyasema hayo jana mahakamani hapo wakati akitoa uamuzi juu ya maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali walimtaka kujitoa kuendelea na shauri hilo kwa madai kuwa mshitakiwa Mwale ambaye ni wakili amefanya kazi Arusha kwa muda mrefu hivyo watakuwa na mwingiliano wa kikazi na wa ule wa kibinafsi na ndugu wa mshitakiwa huyo.

Hakimu huyo aliyesoma uamuzi huo bila upande wa serikali kuwepo mahakamani hapo ambapo alielezea kushangazwa na uamuzi wao wa kutofika bila kuitaarifu mahakama kuwa hawatakuwepo ingawa alisema kuwa kwa mujibu wa sheria kitendo chao hicho hakimzuii kusoma uamuzi huo  kwa kuwa mshitakiwa alikuwepo mahakamani hapo.

Magesa alisema kuwa kwa mara kadhaa tokea shauri hilo limefikishwa mbele ya mahakama hiyo Agosti 9, mwaka jana mawakili wa serikali, Manyanda na Ringo wamekuwa wakidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika kwani kuna nyaraka zinasubiriwa kutoka nchini Marekani jambo alilosema kuwa hizo ni mbinu za kuchelewesha shauri hilo kwani  inashangaza kuona zoezi hilo linachukua muda mrefu kama vile Marekani iko kwenye sayari nyingine.

Aliwataka mawakili wakuu hao wa Serikali, Manyanda na Ringo kukamilisha upelelezi wa shauri hilo ili liweze kuendelea ili kuepusha kutumia vibaya kodi za wananchi kutokana na kuwa mawakili hao wanaoishi jiji Dar es Salaam huwalazimu kusafiri kuja jiji hapa kila mara shauri hilo linapotajwa jambo alilosema kuwa walipa kodi wa nchi hii hawapendi kuona kodi zao zikitumiwa na watu wasio makini na kazi zao kama wanavyofanya huku akitolea mfano wa jana hawakutokea mahakamani hapo bila taaarifa yoyote.

Magesa alisema kuwa hatua ya mawakili hao wakuu wa serikali kuibua hoja ya kutokuwa na imani naye baada ya kutupwa kwa maombi yao mahakama kuu kanda ya Arusha waliyotaka kufanyiwa mapitio uamuzi alioutoa kwa TRA wamrejesheee Mwale magari yake saba kunadhihirisha kuwa walileta maombi hayo baada ya kutopendezwa na maamuzi ya mahakama.

Alisema kuwa kutopendezwa na maamuzi ya mahakama haiwezi kumsababisha hakimu kujitoa kwenye kesi ambapo alinukuu maamuzi mbalimbali ya mahakama ya rufaa ambayo yaliweka wazi kuwa endapo hakimu au jaji atajitoa kwa kuwa tu upande mmoja haukupendezwa na maamuzi ya mahakama itatoa fursa kwa mawakili na waendesha mashitaka kufanya uchaguzi wa mahakimu kama ambavyo watu hupita madukani kuangalia bidhaa kabla ya kuzinunua (window shopping).

“Wanataka hakimu ajitoe kwa kuwa ametoa uamuzi ambao hawakuupenda, kimsingi hiyo haiwezi kuwa sababu ya hakimu kujitoa, mahakama haiwezi kufanya kazi kwa ajili ya kuwafurahisha watu fulani, kama wangekuwa hapa leo ningewaambia mahakama hii haiko kumpandeza yeye (Manyanda)  na Ringo, mahakama hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria haiko kuifurahisha ofisi ya mwanasheria wa serikali au mtu mwingine yeyote” alisisitiza hakimu Magesa.

Alisema kuwa sheria iko wazi kuwa hakimu au jaji anaweza kujitoa kwenye kesi endapo kutatolewa ushahidi wa kuwepo mahusiano ya karibu ,  kindugu au jaji au hakimu kufaidika na uamuzi alioutoa jambo ambalo mawakili hao wa serikali hawakuweza kuleta mahakamani hapo ushahidi wa aina hiyo.

Awali akichambua hoja za mawakili hao wa serikali waliomtaka ajitoe kwenye shauri hilo kwa kuwa Mwale ana ofisi jijini Arusha hivyo watakuwa na mwingiliano wa kikazi, Magesa alisema kuwa hoja hiyo haina msingi kwani hata ofisi ya mwanasheria ina ofisi jijini Arusha na anauhakika ina mwingiliano wa kikazi  na ofisi ya uwakili ya Mwale hivyo nao hawakupaswa kuendesha shauri hilo.

Alisema kuwa inashangaza mawakili hao waliobobea kwenye fani hiyo mpaka kufikia kiwango cha kuwa mawakili wakuu wa serikali kutoa hoja ambazo haziwezi kutolewa na mtu ambaye hajamaliza hata darasa la saba kwani kwenye sheria za uendeshaji mahakama hakuna eneo linasema kuwa mahakama haitasikiliza shauri la mtu mwenye ofisi kwenye eneo husika huku akihoji sababu za wao kufungua shauri hilo kwenye mahakama hiyo wakati wakijua ofisi ya Mwale iko mkoani hapa.

Hakimu Magesa alisema kuwa mahakimu na majaji wanaishi kwenye jamii na hutumia na kushiriki kwenye mambo yote na wanajamii  kwani hakuna barabara , makanisa, misikiti au masoko yaliyotengwa kwa ajili yao hivyo huwezi kutaka wasikutane na ndugu au watu wenye kesi ambao alidai si rahisi kuwajua kwani hawatembei na vibao kuonyesha kuwa wana ndugu zao wenye kesi mahakamani hivyo akadai hoja hiyo ya mawakili wa Serikali ni mgando na  hao wanaozitumia watakuwa wanatumia vitu vingine kufikiri zaidi ya ubongo.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo wakili Mwale pamoja na ndugu zake waliokuwa wamefurika mahakamani hapo walionekana wakikumbatiana huku wakilia kwa furaha ambapo shauri hilo limeahirishwa mpaka julai 13, mwaka huu litakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa

No comments:

Post a Comment