kikundi cha wawada kusomesha watoto wao mpaka chuo kikuu

KIKUNDI cha kusaidiana cha Wawazi Wakweli Daima (WAWADA) cha jijini Arusha kimeweka mikakati kuhakikisha wanasomesha watoto wao kuanzia elimu ya awali mpaka ile ya Chuo Kikuu. Mwenyekiti wa umoja huo, Didas lorouo aliyasema hayo juzi alipokuwa akisoma risala ya kikundi hicho chenye jumla ya wanachama 110 wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa kikundi hicho ambapo mgeni rasmi alikuwa ni diwani wa kata ya Ngarenaro,Isaya Doita. Alisema kuwa wanakikundi hao wanahudumia familia zao zenye zaidi ya watu 800 waishio jijini Arusha hivyo njia pekee ya kuhakikisha familia hizo zinajikwamua kiuchumi ni kuwezesha watoto wao kupata elimu nzuri itakayowawezesha kuajiriwa na kujiajiri kwenye sekta rasmi na zisizo rasmi. “Moja ya masharti yaliyo kwenye katiba yetu ni kuhakikisha watoto wetu wanasoma kutoka shule ya msingi mpaka chuo kikuu kwa kupata mkopo wa riba nafuu na kuhakikisha wanaumoja wanapata msaada pindi wanapopata matatizo hasa ya msiba” alisema Lorouo. Hata hivyo mwenyekiti huyo alisema kuwa changamoto kubwa wanayowakabili kwa sasa ni uwezo mdogo wa kifedha hivyo ku kosa mtaji wa kuwawezesha kuanzisha Chama Cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) hasa kutokana na wengi wa wanachama wao wanajishughulisha na biashara ndogondogo maarufu kama ‘machinga”. Akiongea na wanaWAWADA diwani Doita aliwapongeza kwa kuanzisha umoja huo huku akiwasisitiza kuwekeza nguvu kubwa katika kusaidiana wakati wa uhai na si kusubiri wakati wa kifo kama ilivyojengeka kwenye maeneo mengi nchini ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakijitolea zaidi kugharamia mazishi kwa kununua majeneza yenye gharama kubwa wakati akati marehemu alipokuwa hospitalini kalazwa walishindwa hata kumjulia hali. Alisema kwamba watanzania wanapaswa kuthaminiana wakati wa maish a ya uhai na si kusubiri kumthamini mtu akiwa ndani ya jeneza ambapo alikubali kuwasaidia wanakikundi hao kuweza kusajiliwa hivyo kuwawezesha kunufaika na fedha zinazotengwa na halmashauri kwa ajili ya kusaidia vikundi kama hivyo. Umoja huo ulianza mwaka 2001 ukiwa na wanachama 17 wanaume 10 na wanawake saba ambapo ada ya kiingilio ni shilingi 12,000 huku kila mwezi mwanachama akitakiwa kuchangia shilingi 2,000.

0 Comments:

Post a Comment